Na John Walter-Manyara
Naibu Spika wa Bunge la Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, Mheshimiwa Daniel Sillo, amesema maendeleo hayana chama, dini wala kabila, ndio maana Serikali inaendelea kupeleka fedha za miradi ya maendeleo kila kona ya nchi bila kubagua.
Mheshimiwa Sillo ameyasema hayo alipokuwa mgeni rasmi katika ibada maalum ya shukrani kwa ajili ya Shule mpya shikizi ya Ayaaben iliyopo Kata ya Qameyu, Kijiji cha Endaw, pamoja na uzinduzi wa shule hiyo mpya ya msingi.
Amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata haki yake ya msingi ya elimu, bila kujali anapotoka au anapoishi, akisisitiza kuwa miradi ya maendeleo inalenga kuleta usawa na kuboresha maisha ya wananchi wote.
Shule hiyo imejengwa kwa juhudi za wananchi wa kijiji kwa kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali, ikiwa na miundombinu inayojumuisha madarasa mawili, ofisi moja pamoja na vyoo vya wanafunzi.
Lengo kuu la ujenzi wa shule hiyo ni kuwapunguzia mzigo wanafunzi waliokuwa wakitembea umbali mrefu kufuata elimu katika Shule ya Msingi Endaw ambayo ndiyo shule mama.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mheshimiwa Daniel Sillo amewapongeza wananchi kwa mshikamano na moyo wa kujitolea waliouonyesha katika kuchangia ujenzi wa shule hiyo, akibainisha kuwa ushirikiano kati ya wananchi na Serikali ndio msingi wa maendeleo ya kweli.
“Maendeleo hayana chama. Pale wananchi wanapoungana na Serikali, matokeo yake ni mazuri kama haya tunayoyaona leo. Hii ni hatua kubwa kwa mustakabali wa elimu ya watoto wetu,” amesema Sillo.
Ujenzi wa shule hiyo umegharimu jumla ya Shilingi Milioni 66, ambapo wananchi wamechangia Shilingi Milioni 37.5, Serikali Kuu imetoa Shilingi Milioni 25, Mfuko wa Jimbo umechangia Shilingi Milioni 3, huku wadau wakichangia jumla ya Shilingi laki nne na elfu themanini.
Aidha, Mheshimiwa Sillo ameahidi kuiletea shule hiyo vifaa vya michezo kwa ajili ya mazoezi na kuendeleza vipaji vya wanafunzi, pamoja na kuisapoti shule kwa madawati yenye thamani ya Shilingi laki tisa ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Ibada ya shukrani iliongozwa na Askofu Elisante Naman wa Kanisa la Disciple Nations Pentecost Church (DNPC), ambapo waumini na wananchi wa Kijiji cha Endaw walimshukuru Mungu kwa hatua hiyo kubwa ya maendeleo katika sekta ya elimu.
Katika ibada hiyo waliombea pia Taifa la Tanzania, wakimuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aendelee kuiongoza nchi kwa hekima, amani na usalama.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Qameyu amemshukuru Mheshimiwa Daniel Sillo kwa ushirikiano wake wa karibu na mchango mkubwa katika kusimamia na kuunga mkono miradi ya maendeleo, hususan katika sekta ya elimu, akisema shule hiyo mpya shikizi ya Ayaaben itakuwa mkombozi mkubwa kwa watoto wa eneo hilo.
Shule mpya shikizi ya Ayaaben, ambayo shule mama yake ni Shule ya Msingi Endaw, inatarajiwa kuongeza wigo wa upatikanaji wa elimu, kupunguza utoro, kupunguza umbali wa kutembea kwa wanafunzi na kuongeza ari ya kusoma kutokana na ukaribu wake na makazi ya wananchi.
0 Maoni