Na John Walter-Manyara
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, amezindua rasmi
namba ya bure ya huduma kwa mteja itakayokuwa ikitumika kupokea changamoto,
kero na malalamiko ya wananchi wa mkoa wa Manyara.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Sendiga amesema
namba hiyo ambayo ni 0800 787 722 imelenga kurahisisha upatikanaji wa taarifa
kutoka kwa wananchi kwa wakati, ili changamoto zinazowakabili ziweze
kushughulikiwa kwa haraka na ufanisi. Ameeleza kuwa mwananchi atakuwa na uhuru
wa kupiga namba hiyo bila malipo au makato yoyote na kutoa taarifa sahihi bila
kudanganya.
“Mfumo huu utaimarisha uwajibikaji na uwazi katika utoaji wa
huduma kwa wananchi, kwani utasaidia serikali kupata taarifa za moja kwa moja
kutoka kwa wananchi na kuzifanyia kazi kwa wakati,” amesema Sendiga.
Aidha, Mkuu wa Mkoa amezitaka ofisi zote zilizo chini ya
uongozi wake kuhakikisha zinashughulikia kwa haraka changamoto zote
zitakazopokelewa kupitia namba hiyo. Ameelekeza kuwa baada ya kuzifanyia kazi,
taarifa hizo zirudishwe katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya kuhifadhi
kumbukumbu, maandalizi ya ripoti na ufuatiliaji wa taarifa za kila mwezi.
Uzinduzi wa namba hiyo ya bure unatarajiwa kuongeza ufanisi
katika utoaji wa huduma za serikali na kuimarisha ushirikiano kati ya wananchi
na viongozi katika Mkoa wa Manyara.

0 Maoni