Na John Walter-Hanang'
Mtoto wa miaka minne, Abdilahi Hussein, amefariki dunia leo baada ya kugongwa na gari katika Kijiji cha Endagaw, Kata ya Endagaw, Wilaya ya Hanang mkoani Manyara.
Kwa
mujibu wa taarifa zilizothibitishwa, tukio hilo limetokea wakati mtoto huyo akitoka
nyumbani kwao kuelekea dukani kwao, ambalo lipo upande wa pili wa barabara kuu
inayoelekea Singida.
Akithibitisha
kutokea kwa tukio hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Endagaw, Rajabu Mande, amesema
kuwa kifo cha mtoto huyo ni pigo kubwa kwa jamii, akieleza kuwa mtoto huyo
alikuwa nguvu kazi ya taifa la kesho, lakini maisha yake yamekatizwa kutokana
na dereva kushindwa kuchukua tahadhari katika eneo la makazi ya watu.
Taarifa
zinaeleza kuwa mtoto huyo aligongwa akiwa pembeni ya barabara, na baadaye alikanyagwa
maeneo ya kichwani, hali iliyosababisha kifo chake papo hapo.
Mashuhuda
wa tukio hilo wameeleza masikitiko yao na kuomba mamlaka husika kuchukua hatua
kali dhidi ya madereva wasiotii sheria za usalama barabarani, hasa katika
maeneo yenye makazi ya watu, ili kuzuia ajali zinazogharimu maisha ya wananchi
wasio na hatia.
Jamii
ya Endagaw imeendelea kuomboleza msiba huo, huku wito ukitolewa kwa madereva
wote kuongeza umakini na kuzingatia sheria za barabarani ili kulinda maisha ya
watoto na watumiaji wengine wa barabara.
0 Maoni