F Rose Muhando Alalamikia Kudhulumiwa Mapato na Sony Music Africa | Muungwana BLOG

Rose Muhando Alalamikia Kudhulumiwa Mapato na Sony Music Africa


Na John Walter

Msanii maarufu wa nyimbo za injili nchini, Rose Muhando, amevunja ukimya wake baada ya zaidi ya miaka 15 ya madai ya kudhulumiwa haki yake ya mapato, akieleza malalamiko hayo kupitia ukurasa wake wa Instagram. Katika ujumbe huo, Rose ameeleza kusikitishwa na kile alichokiita ukandamizaji wa haki zake za kifedha unaohusishwa na kampuni ya #SonyMusicAfrica.

Kwa mujibu wa Rose Muhando, licha ya kuacha kufanya kazi na kampuni hiyo kitambo, hadi sasa Sony Music Africa bado inashikilia zaidi ya kazi zake 37, ambazo zinaendelea kutumika kwenye majukwaa mbalimbali ya kidijitali bila yeye kulipwa hata senti moja. 

Amesema hali hiyo ni ya kuumiza zaidi kwa kuwa kazi hizo ni matokeo ya jasho na maisha yake yote ya sanaa.

Katika maelezo yake, Rose ameandika kuwa kwa muda mrefu amekuwa akinyamaza na kuvumilia, akiamini haki yake ingetendeka, lakini maumivu na ukimya wa muda mrefu vimemlazimu sasa kusema wazi. 

Amefafanua kuwa amekuwa akidhulumiwa mapato yake kwenye majukwaa yote ya kidijitali kutokana na ushirikiano wake wa zamani na Sony Music Africa.

Aidha, amebainisha kuwa Serikali kupitia COSOTA Tanzania imejaribu kusimamia na kumsaidia kupata haki yake, lakini juhudi hizo zimekwamishwa kutokana na kile alichodai kuwa ni kukosa ushirikiano kutoka kwa mwakilishi wa Sony Music Africa, Seven Mosha, ambaye anadaiwa kuitwa mara kadhaa bila kutoa ushirikiano unaohitajika.

Rose Muhando amesema hali hiyo imemuumiza na kumvunja moyo, huku akionya kuwa ni mfano wa changamoto zinazowakumba wasanii wengi ambao kimyakimya wanaendelea kudhulumiwa haki zao

Kwa unyenyekevu, ameiomba Serikali kuingilia kati suala hilo, akimtaja moja kwa moja Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Paul Christian Makonda, ili haki itendeke kwa haraka.

Katika hitimisho la ujumbe wake, Rose Muhando amesema amechoka kuvumilia na kunyamaza, akisisitiza kuwa jasho la msanii linapaswa kuheshimiwa na ndoto za wasanii zisikandamizwe. 

Kauli yake imeibua mjadala mpana mitandaoni kuhusu haki za wasanii na usimamizi wa mapato ya kazi za sanaa katika majukwaa ya kidijitali.

Chapisha Maoni

0 Maoni