Habari kutoka Dodoma
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi
Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amesema kuanzishwa kwa sekretarieti ya
utekelezaji wa Sera ya Wazee ya Mwaka 2003 Toleo la Mwaka 2024 ni hatua muhimu
ya Serikali katika kuweka mifumo thabiti ya uratibu, ufuatiliaji na tathmini ya
utekelezaji wa Sera ya hiyo katika ngazi zote za utawala.
Akizungumza na
Sekretarieti ya Uratibu wa Utekelezaji wa Sera hiyo kwa njia ya mtandao
kidijitali tarehe 16 Januari, 2026, jijini Dodoma amesisitiza kuwa sekretarieti
itakuwa kiungo muhimu kati ya Wizara za Kisekta, Taasisi za Umma, Mamlaka za
Serikali za Mitaa na wadau wa maendeleo katika kuhakikisha huduma zinazowalenga
wazee zinapangwa na kutekelezwa kwa ufanisi na kwa kuzingatia mahitaji halisi
ya walengwa.
Aidha, ametoa wito kwa Wizara za Kisekta, Mikoa na
Halmashauri kuhakikisha masuala ya wazee yanaingizwa kikamilifu katika mipango
na bajeti zao za kila mwaka, pamoja na kuwasilisha taarifa za utekelezaji kwa
wakati huku akisisitiza kuwa mafanikio ya Sera ya Wazee yatategemea dhamira ya
pamoja ya Serikali na wadau wote katika kuwajali, kuwathamini na kuwalinda
wazee kama hazina ya Taifa.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi, amewataka waratibu wa
masuala ya wazee kuhakikisha wanasimamia kikamilifu utekelezaji wa Sera ya
Taifa ya Wazee kwa vitendo badala ya kubaki kwenye maandiko pekee.
“Ni dhahiri kuwa tunalo jukumu la pamoja la kuhakikisha Sera
ya Taifa ya Wazee inatekelezwa kwa vitendo na kwa ufanisi katika Wizara za
kisekta na taasisi zetu. Ushirikiano, uwajibikaji na uratibu wa karibu ndiyo
msingi wa kufanikisha dhamira hii” amesema Mhe. Maryprisca
Kikao hicho kimejumuisha wadau kutoa katika Wizara za Kisekta, Mikoa,
Wilaya na Majukwaa mbalimbali pamoja na
mambo mengine imezinduliwa Sekretarieti ya Kitaifa ya utekelezaji wa Sera hiyo.
0 Maoni