Na John Walter-Manyara
Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeendelea kutekeleza miradi ya ujenzi wa madaraja katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo kwa lengo la kurahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi kwa wananchi, hususan kipindi cha mvua.
Akizungumza kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo, Meneja wa
TARURA Wilaya ya Mbulu, Mhandisi Nuru Hondo amesema jumla ya shilingi bilioni
1.4 zimetolewa na Benki ya Dunia (World Bank) kwa ajili ya ujenzi wa madaraja
matatu ambayo ni daraja la Isale, Marish pamoja na Haydom 102 ndani ya Wilaya
ya Mbulu.
Amesema miradi hiyo inalenga kuondoa changamoto ya
mawasiliano na usafirishaji ambayo imekuwa ikiathiri wananchi kwa muda mrefu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Dudiyek Kata ya
Imboru, Paskali Thomas amesema wananchi wanasubiri kwa hamu kukamilika kwa
mradi wa ujenzi wa daraja katika maeneo hayo akibainisha kuwa kipindi cha mvua
wamekuwa wakipata mateso makubwa kutokana na kukosa huduma muhimu kama afya,
elimu na masoko kwa sababu ya kukatika kwa mawasiliano.
“Msimu wa mvua tunateseka sana, hatuwezi kuvuka, wagonjwa
wanashindwa kufika hospitali, wanafunzi wanashindwa kwenda shule na hata
shughuli za kiuchumi zinasimama.
Tunashukuru TARURA kwa kutusikiliza na tunasubiri kwa
matumaini makubwa mradi huu,” amesema Paskali Thomas.
Aidha, ameipongeza TARURA kwa usimamizi mzuri wa miradi hiyo
na kuhakikisha inatekelezwa kwa viwango vinavyotakiwa.
Ameongeza kuwa miradi hiyo imechangia kutoa ajira kwa vijana
wa eneo hilo, ambapo zaidi ya shilingi milioni 400 zimetumika katika mradi wa
World Bank, hatua inayosaidia kuinua kipato cha wananchi na kupunguza tatizo la
ukosefu wa ajira.
Wakati huo huo, Meneja wa TARURA Mkoa wa Manyara, Mhandisi
Salim Bwaya, alifanya ziara ya kukagua miradi hiyo akiambatana na menejimenti
nzima ya TARURA mkoa, kwa lengo la kujionea hatua mbalimbali za
utekelezaji.
Katika ziara hiyo, aliwasisitiza wakandarasi kuhakikisha
wanakamilisha ujenzi wa madaraja kwa wakati uliopangwa na kwa ubora unaotakiwa
ili wananchi waweze kunufaika na miradi hiyo kwa haraka.
Mhandisi Bwaya amesema ujenzi wa madaraja hayo ni sehemu ya
jitihada za Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, hususan World
Bank, katika kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja ili kuchochea
maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika maeneo ya vijijini.
Miradi ya madaraja inayoendelea katika Wilaya ya Mbulu
inatarajiwa kuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi, kwa kuboresha usafiri, kuongeza
upatikanaji wa huduma za jamii na kuimarisha shughuli za kibiashara katika
ukanda huo wa Mkoa wa Manyara.
PICHA MBALIMBALIU WAKATI WA ZIARA HIYO.
0 Maoni