F Jamii Yatakiwa Kukemea Ukatili wa Kijinsia, Malalamiko ya Wanaume Kutokusikilizwa Polisi Yaibuliwa | Muungwana BLOG

Jamii Yatakiwa Kukemea Ukatili wa Kijinsia, Malalamiko ya Wanaume Kutokusikilizwa Polisi Yaibuliwa


Na John Walter-Babati

Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Wilaya ya Babati, Januari Bikuba, ametoa wito kwa jamii kukemea kwa nguvu vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuhakikisha wahusika wanachukuliwa hatua za kisheria bila upendeleo.

Akizungumza Februari 12, 2026 katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Magugu, Bikuba amesema ukatili wa kijinsia haufai kufumbiwa macho hata kidogo na kuwataka wananchi kuendelea kutoa taarifa za matukio hayo bila kusahau kutumia namba ya msaada 116.

Katika mkutano huo, baadhi ya wanaume wameeleza kuwepo kwa changamoto kwa waathirika wa ukatili, hususan wanaume, wakidai kuwa wanapofika vituo vya polisi kutoa taarifa mara nyingine hawasikilizwi na wakati mwingine kufukuzwa.

Bikuba ameisisitiza kuwa matukio ya ukatili wa kijinsia ni uhalifu kama ilivyo kwa makosa mengine ya jinai, hivyo jamii inapaswa kutoa taarifa mapema na kuwa tayari kutoa ushahidi mahakamani ili sheria iweze kuchukua mkondo wake dhidi ya wahusika.

Ameongeza kuwa mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia yanahitaji ushirikiano wa wadau wote, wakiwemo viongozi wa jamii, familia na vyombo vya dola, ili kuhakikisha kila mwathirika anapata haki bila kujali jinsia yake.

Aidha, amewahimiza wananchi kuachana na tabia ya kuficha matukio ya ukatili majumbani, akieleza kuwa kufanya hivyo kunachangia kuendelea kwa vitendo hivyo na kudhoofisha juhudi za serikali za kulinda haki za binadamu.

Naye mkuu wa Kituo cha Polisi Magugu amesema baadhi ya waathirika wa ukatili hushindwa kufuatilia kesi hadi mahakamani kutokana na kupewa hongo, hali inayokwamisha mwenendo wa mashauri na wakati mwingine kusababisha kesi kuondolewa kabisa mahakamani.

 

Chapisha Maoni

0 Maoni