Na John Walter-Babati
Mkuu wa Wilaya ya Babati na Mwenyekiti wa Kamati ya
Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo, Emmanuela Kaganda, amesema wanafunzi
waliokuwa wakishikiliwa kwa tuhuma za kumshambulia mwenzao hadi kufariki dunia
wameachiwa huru na sasa wanaendelea na maisha yao ya kawaida.
Akizungumza wakati akihitimisha hotuba yake katika hafla
ya kuwapongeza walimu waliofundisha kidato cha nne mwaka 2025 katika
Halmashauri ya Wilaya ya Babati kwa kufanikisha matokeo mazuri ya wanafunzi,
Kaganda ameupongeza uongozi wa Jeshi la Magereza Wilaya ya Babati kwa mchango
wao katika malezi na elimu ya wanafunzi hao.
Amesema kulikuwa na wanafunzi waliokinzana na sheria na
kuhifadhiwa katika mazingira ya uangalizi maalum, akitolea mfano tukio
lililotokea katika Shule ya Sekondari Qash, ambapo wanafunzi hao waliendelea
kupata fursa ya kusoma na kufanya mitihani yao chini ya usimamizi wa karibu wa
maafisa elimu, uongozi wa magereza na walimu.
“Kuna watu waliona lile ni eneo baya, lakini ni eneo la
urekebishaji, watoto wamekaa pale, wamesoma na kufanya vizuri katika
mitihani—wapo waliopata daraja la kwanza na la pili, hakuna aliyepata sifuri, kama
wangetelekezwa tungewanyima haki yao ya msingi ya elimu,” alisema Kaganda.
Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya ofisi ya elimu, Jeshi
la Magereza na walimu uliwezesha wanafunzi hao kufanya mitihani kwa mafanikio,
na sasa wameachiwa huru na wanaendelea na masomo na maisha yao kwa utulivu.
Mnamo Agosti 16, 2025, zaidi ya wanafunzi kumi walikuwa
wakishikiliwa kwa tuhuma za kumuua mwenzao, Yohana Konki (17), kwa madai ya
wizi wa kishkwambi, tukio lililoshtua jamii ya Wilaya ya Babati.
0 Maoni