Na John Walter-Babati
Wananchi wa Kijiji cha Matufa, Kata ya
Magugu wilayani Babati mkoani Manyara, wameanza ujenzi wa zahanati kwa nguvu
zao wenyewe baada ya kukosa huduma za afya kwa muda mrefu katika eneo hilo.
Wakizungumza wakati wa kuanza kwa ujenzi
huo, wananchi wamesema kwa sasa wanalazimika kusafiri umbali mrefu kufuata
huduma za afya katika Kijiji jirani cha Mawemairo au Kituo cha Afya Magugu,
hali inayowalazimu kutumia muda na gharama kubwa.
Wameeleza kuwa wanatamani huduma hiyo
iwe karibu zaidi ili kurahisisha upatikanaji wa matibabu, hasa kwa watoto,
wazee na wajawazito.
Diwani wa Kata ya Magugu, Stanley
Charles, ameungana na wananchi katika kuchimba msingi wa ujenzi wa zahanati
hiyo ikiwa ni ishara ya kuunga mkono juhudi zao.
Amesema wanamshukuru Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan kwa kuendelea kupeleka miradi mbalimbali ya maendeleo nchini,
huku akiomba serikali na wadau wengine wa maendeleo kuisapoti jamii ya Matufa
ili kukamilisha ujenzi huo kwa wakati.
Kwa mujibu wa takwimu za kijiji hicho,
zahanati hiyo itawanufaisha zaidi ya wananchi 6,722 wanaoishi katika kaya
1,943.
Shabani Mpondo, mmoja wa wakazi wa
kijiji hicho, amesema wananchi wameamua kujitolea michango yao ya fedha, nguvu
kazi na vifaa ili kuhakikisha wanapata huduma ya afya ndani ya kijiji chao.
Ameongeza kuwa Matufa ni kijiji cha pili
kwa ukubwa katika Kata ya Magugu baada ya Magugu, hivyo mahitaji ya huduma za
afya ni makubwa.
Wakina mama wa kijiji hicho wamesema
kukamilika kwa zahanati hiyo kutakuwa msaada mkubwa hasa wanapohitaji
kujifungua nyakati za usiku, ambapo kwa sasa hulazimika kusafiri umbali mrefu
katika mazingira yasiyo salama.
Ujenzi wa zahanati hiyo unaonesha
dhamira ya wananchi kushiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo yao, huku
wakitarajia kupata msaada wa serikali na wadau ili kufanikisha mradi huo muhimu
kwa ustawi wa jamii.
0 Maoni