Lakini zaidi nimeongeza imani yangu kwa Lowassa baada ya
kubaini kuwa hata Baba wa Taifa Julius Kambarage Nyerere alimuona kama kijana
makini mwenye maono na dhamira safi
ya kuwatumikia Watanzania. Mwaka 1995 wakati Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi
anamaliza muda wake mwandishi wa habari Mwita Matinyi alimuliza Mwalimu Nyerere
alikuwa anafikiri ni nani angeweza kumrithi Mwinyi kuiongoza Tanzania .
Mwalimu alijibu Matinyi hivi. Nanukuu: Ni kweli Mzee Mwinyi
anaondoka lakini ndani ya CCM kuna viongozi wengi wenye sifa za kuwaongoza
Watanzania, kikubwa tu awe na dhamira kwa mfano wapo wakina Warioba, Mzee Msuya
na Mark Bomani na wapo vijana hodari na wenye upeo mkubwa sana kama Mkapa,
Kikwete na Lowassa ni jambo la heri sana CCM kuwa na watu kama hawa (Majira
26/5/1995) ukurasa wa 3; na Nipashe 26/5/95 ukurasa wa 3).
Pia nikiwa ripota Radio Tanzania Dar es Salaam niliwahi
kufanya kazi na Lowassa katika miaka ya 90. Nilivyouona utendaji wake wa kazi
zama hizo nashawishika kwamba anafaa kuwa kiongozi wa nchi yetu. Nilishuhudia
akijituma kweli kweli kwenye kazi za umma zama hizo.
Kadhalika namuunga mkono Lowassa kwa sababu hagombei Urais
kupitia chama cha CCM ambacho kinakumbatia mfumo wa kuwadharau na kuwafukarisha
wananchi huku watawala wachache wakineemeka kwa kutumia rasilimali za nchi kama
vile nchi hii ni mali
ya watawala, familia zao na marafiki zao.
Ninaamini kwa kugombea Urais kupitia UKAWA, CCM itapunguziwa
dharau na jeuri yake dhidi ya wananchi ambao ndio wenye mamlaka ya mwisho
kuhusu hatma ya nchi yetu. Mfano CCM mwaka jana 2014 ilionyesha dharau kubwa sana kwa wananchi kwa
kuizika Rasimu ya Katiba iliyotengenezwa kwa kutumia maoni ya wananchi wakati
fedha zaidi ya bilioni 130 zilitumika. Kwa kutumia mabilioni hayo bila Katiba
Mpya kupatikana ni kufisadi mali
za wananchi mchana kweupe. Haikubaliki.
Vile vile namuunga mkono Lowassa kwa kwa sababu anaukataa
hadharani umaskini wa kuchongwa ambao watawala wanautumia kwa faida yao ili
waendelee kuwanunua wananchi mafukara wakati wa uchaguzi na wakishapata
madaraka waendelee kujineemesha na mali za nchi.
Nchi yetu siyo maskini bali watawala wanaendekeza matakwa ya
wawekezaji (wakoloni wa zama hizi za utandawazi wizi) ambao wanaliibia taifa
rasilimali nyingi na na hatimaye nchi za wawekezaji hao (donors)wanawapoza
watawala kwa vijimisaadaa uchwara. Ni aibu sana
kwa kiongozi wa Tanzania
kijipitisha nchi moja hadi nyingine Marekani, Ulaya ,
China , India na Ausralia n.k kutembeza bakuli (omba
omba kama matonya vile) huku nchi yetu ikiwa
na rasilimali tele. Tena wakati watawala wanakwenda kuomba eti wanapanda ndege
daraja la kwanza. Huu ni wenda wazimu. Ni kuiaibisha Tanzania na Afrika.
Sina chama cha siasa ninachofungamana nacho kwa sasa, lakini
namuunga mkono Lowassa kugombea Urais kupitia UKAWA kwa sababu naamini akiwa
Rais wa nchi yetu upuuzi huu wa kuendekeza umaskini kwa kuomba omba nchi za nje
huku tukitoa mali za nchi honyo hovyo kwa wageni na kuamini kuwa maendeleo ya
nchi yetu yataletwa kwa misaada kutoka nje, kutakomeshwa. Naamini hata hao
wakoloni wa zama hizi za utandawazi wizi wanajua Lowassa hatachekacheka nao.
Lakini zaidi namuunga mkono Lowassa kwa sababu Watanzania
wakiridhia kwenye sanduku huru la kura hapo Oktoba awe Rais wa Tanzania ,
vyama vinavyounda UKAWA vitasimamia kuhakikisha kuwa mamlaka ya wanannchi
hayaporwi hovyo hovyo tena.
Kwa hiyo Rasimu ya Katiba ya wananchi itaheshimiwa na nchi
yetu itapata Katiba Mpya inayotokana na maoni ya wananchi. Kwa kufanya hivyo
taifa hili litaanza kupiga hatua kubwa ya kuondoa ufukarishwaji wa wananchi
walio wengi unaofanya na watawala wa CCM kwa kushirikiana na wakoloni wa zama
hizi za utandawazi