Raia wa Burundi
wamepatwa na hali ya wasiwasi mkubwa juu ya uwezekano wa kuibuka vita vya ndani
vitakavyoambatana na mauaji makubwa nchini humo.
Kwa mujibu wa televisheni ya Ufaransa, mauaji ya Jenereali
Adolphe Nshimirimana aliyekuwa mtu wa karibu wa Rais Pierre Nkurunziza,
yamezidisha wasiwasi mkubwa kwa raia wa nchi hiyo masikini ya Afrika ya kati
juu ya kutokea vita vya ndani nchini humo.
Raia wa Burundi wana wasiwasi kwamba,
wafuasi wa Nshimirimana watachukua hatua ya ulipizaji kisasi dhidi ya wapinzani
wa kisiasa wa serikali na hivyo kuibuka kwa vita. Kufuatia hali hiyo, anga ya
usalama nchini Burundi
imekuwa tete, wakati huu ambapo fikra za wananchi zinafuatilia nini kitatokea
baada ya tukio hilo .
Jenereali Adolphe Nshimirimana aliuawa pamoja na dereva wake
asubuhi ya jana baada ya maroketi mawili kulenga gari lake
kabla ya kumiminiwa risasi katika eneo
la Kamenge mjini Bujumbura .
Adolphe Nshimirimana aliwahi kuwa mkuu wa majeshi na alikuwa akifanya kazi
katika ikulu ya Rais Nkurunziza. Wapinzani wa serikali wanamtaja Nshimirimana
kuwa aliyekuwa na mchango mkubwa katika kumsafishia njia Rais Pierre Nkurunziza
kusalia madarakani na kwamba, kama si yeye
basi rais huyo asingeweza kugombea muhula wa tatu wa urais.
