ZFA wamkalia kooni Malinzi

Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kimemtaka rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi kuomba radhi kwa kauli yake wanayodai kuwa ya kibaguzi na uchochezi dhidi ya chama hicho na wajumbe wake.

Chama hicho kinachosimamia soka visiwani Zanzibar kimekwenda mbali na kudai kuwa Malinzi asipofanya hivyo watamfungulia kesi mahakamani.

Wiki iliyopita, Malinzi aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa haitambui Kamati ya Muda ya ZFA inayosimamia shughuli za michezo visiwani humo na kwamba anamtambua mtu mmoja pekee ambaye ni rais wa ZFA, Ravia Idarous Faina.

Viongozi hao wa Zanzibar ambao walionekana kukerekwa na kauli hiyo ya Malinzi walisafiri hadi Dar es Salaam na jana asubuhi katika kikao chao na waandishi wa habari, makamu wa rais wa ZFA, Alhaji Ameir Haji alisema kuwa anashangazwa na kauli ya Malinzi wakati yeye alihusika kuunda kamati hiyo anayoipinga na kuwapotosha wananchi.

“Yeye alikuwa Mwenyekiti wa kikao hicho, leo hii anasema haitambui,  hatuamini kama uamuzi aliotoa wa kutoitambua kamati hiyo ameufanya peke yake na siyo TFF nzima. Tunamtaka aombe radhi kuanzia sasa akishindwa ni lazima tumfungulie kesi kwa uchochozi na ubaguzi kwani Zanzibar na Bara wote ni Muungano mmoja, TFF siyo sehemu ya ZFA ila ZFA ni sehemu ya TFF.

“Tangu Malinzi aingie madarakani kuna mambo mengi yamekuwa yakifanywa kinyume na utaratibu za Fifa ikiwamo kutotendewa haki sisi, lakini tulikuwa hatupendi kuyazungumza. Hivyo anapaswa kuwa kiongozi bora wa michezo tofauti na anakokwenda sasa anapotoka na kuharibu kabisa mpira wa Tanzania,” alisema Ameir.

Mwanasheria wa ZFA, Abdallah Juma alisema, “Malinzi amekuwa akiyafanya mengi ambayo tuna ushahidi nayo, ambayo ni ya kutuharibia. Tulijuwa angekuwa mtu wa kuisaidia Zanzibar kama alivyoahidi alipoalikwa kwenye kikao cha ZFA. Tunaomba Malinzi afute kauli yake ya upotoshaji tuna mambo mengi ya ushahidi endapo tutafika mahakamani.”
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items