Diamond Platnumz Awagusa Wafanyabiashara Tarime, Atoa Mitaji ya Kuinua Biashara Zao.



Na Timothy Itembe, Tarime.


WAFANYABIASHARA wadogo wadogo wa Soko Jipya la Rebu, wilayani Tarime, mkoani Mara, wamempongeza mwanamuziki maarufu nchini, Diamond Platnumz, kwa kuwasaidia mitaji ya biashara zao kupitia msaada wa fedha tasilimu alioutoa leo.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wafanyabiashara walionufaika na msaada huo walisema wamefurahishwa na kitendo cha msanii huyo kuwafikia na kuwapa mtaji ambao utawasaidia kuimarisha biashara zao pamoja na kuongeza kipato cha familia zao.


Maryam Maduhu, ambaye anajishughulisha na biashara ya mahindi ya kuchemsha, alisema kabla ya kupata msaada huo mtaji wake ulikuwa umedorora, hali iliyokuwa ikimkwamisha kuendeleza biashara yake.alisema kupokea shilingi 100,000 kutoka kwa Diamond Platnumz kumempa matumaini mapya ya kukuza biashara yake.


"Tunamshukuru Mwenyezi Mungu na tumbo la mama aliyembeba na kumzaa Diamond Platnumz. Mungu ambariki kwa kutuunga mkono katika mitaji yetu. Familia zetu zimepata faraja na matumaini mapya," alisema Maryam.


Naye Rhobi Chacha, mfanyabiashara wa nyanya katika soko hilo, alisema kiasi cha shilingi 70,000 alichopata kitamsaidia kuongeza mtaji wake ambao hapo awali ulikuwa umeyumba alisema msaada huo utamwezesha kufanya biashara kwa ufanisi zaidi na kuongeza kipato chake, huku akimshukuru Diamond Platnumz kwa moyo wake wa kusaidia jamii.


Akizungumza wakati wa utoaji wa msaada huo, Diamond Platnumz alisema anaamini katika kurejesha kwa jamii sehemu ya baraka alizojaliwa na Mungu kwa kuwasaidia wenye uhitaji.

Alisema dini na maadili vinahimiza kuwajali masikini, yatima na watu wenye mahitaji maalumu, hivyo ataendelea kushiriki katika shughuli za kijamii zinazolenga kuboresha maisha ya wananchi.


Katika shughuli hiyo, Diamond Platnumz aliambatana na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (MNEC), Christopher Mwita Ghachuma, ambaye alikuwa mwenyeji wake.


Kwa upande wake, Ghachuma aliwataka wafanyabiashara waliopokea fedha hizo kuzitumia kama mitaji ya biashara zao badala ya matumizi mengine, ili ziwe chachu ya kuongeza kipato na kuboresha maisha yao.


Aidha, aliwasisitiza kuendelea kudumisha amani na utulivu nchini, akieleza kuwa mazingira ya amani ndiyo msingi wa ukuaji wa biashara na maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi.

,,,,,,,,,,,,mwisho,,,,,,,

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi