Na Timothy Itembe, Serengeti.
MKOA wa Mara umeendelea kujipanga kuimarisha sekta ya tumbaku kwa lengo la kuwa kitovu cha uzalishaji wa zao hilo nchini, huku viongozi wa serikali, vyama vya ushirika na wadau wa sekta hiyo wakisisitiza ushirikiano, uwajibikaji na mikakati ya kuongeza tija kwa wakulima.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa WAMACU Ltd, Momanyi Range, wakati akifungua Mkutano wa Pili wa Vyama Wanachama wa WAMACU Ltd unaowakutanisha wadau wa zao la tumbaku mkoani Mara.
Range alisema mkutano huo ni mwendelezo wa utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa katika mkutano wa kwanza, ambao ulifanyika mwaka 2025 juni ukiwa na lengo la kuifanya Mara kuwa mkoa wa mfano katika uzalishaji wa tumbaku nchini Tanzania.alieleza kuwa mkutano huo umezikutanisha wilaya za Serengeti, Tarime na Rorya, huku wilaya nyingine zikitarajiwa kushiriki katika mikutano ijayo.
"Natumia nafasi hii kuwapongeza wadau wote wanaofanikisha mkutano huu pamoja na maendeleo ya kilimo cha tumbaku mkoani Mara.Pia nawapongeza viongozi wa WAMACU kwa kuhakikisha ushirika unajumuisha jinsia zote, pamoja na wadau wetu wakubwa akiwemo Benki ya NMB,CRDB na Alliance One," alisema Range.
Naye Afisa kilimo mwandamizi na Meneja wa Tumbaku Mkoa wa Mara, Sosthenes Kikwelele, alisema Wilaya ya Serengeti imeendelea kufanya vizuri katika uzalishaji wa tumbaku na imechangia kwa kiasi kikubwa Mkoa wa Mara kuingia miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa uzalishaji wa zao hilo nchini.
Alisema tumbaku ni moja ya mazao muhimu ya biashara yanayoingiza fedha za kigeni na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa pamoja na kuinua kipato cha wakulima na kuwa msimu wa mwaka huu wanatarajia kufanya kazi na wakulima 928, hatua inayotarajiwa kuongeza uzalishaji na kuimarisha uchumi wa wakulima.
Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Angelina Marco Lubela,aliwapongeza wakulima wa tumbaku kwa juhudi walizoonyesha licha ya changamoto zilizojitokeza katika msimu uliopita.alisema kupitia uzalishaji wa kilo milioni 3.38 za tumbaku, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti imekusanya ushuru wa Dola za Marekani 186,000, huku vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) vikikusanya Dola 281,000, sawa na zaidi ya shilingi milioni 600.
Aidha, aliwataka viongozi wa AMCOS kuhakikisha wanawalipa wakulima madeni yao kwa wakati ili kurejesha imani na tabasamu kwa wananchi, sambamba na kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassani za kuboresha maisha ya Watanzania.
Akisoma risala kwa mgeni rasmi, Meneja Mkuu wa WAMACU Ltd, Samwel Gisiboye,alisema mkutano huo umeandaliwa kwa lengo la kutathmini utekelezaji wa maelekezo na miongozo ya serikali, pamoja na kuweka mikakati ya kuongeza uzalishaji wa tumbaku wenye tija katika msimu wa 2026/2027.
Akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo, mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Dkt. Alfani Haule, alisema bado kuna changamoto zinazokwamisha maendeleo ya sekta hiyo, ikiwemo uzalishaji mdogo na ucheleweshaji wa malipo ya wakulima.
Aliwataka wadau kuongeza juhudi katika kuhamasisha kilimo bora cha tumbaku kwa kuzingatia kanuni na taratibu zote za uzalishaji ili kuongeza mavuno na ubora wa zao hilo.
Dkt. Haule pia alisisitiza umuhimu wa kutolewa kwa kalenda rasmi ya msimu wa tumbaku pamoja na tarehe za kufunguliwa kwa soko,akisema hatua hiyo itasaidia wafadhili Benk kutoa fedha kwa wakati ili kudhibiti utoroshaji wa tumbaku kwenda nje ya nchi.
Alibainisha kuwa shinikizo la mahitaji ya kifedha wakati wa kufunguliwa kwa shule limekuwa likiwalazimu baadhi ya wakulima kuuza tumbaku kupitia njia zisizo rasmi ili kupata fedha za ada na matumizi mengine ya watoto wao.

