Na Timothy Itembe Tarime..
TIMU ya Tarime All Star imeibuka bingwa wa Ligi ya Polisi Jamii Cup 2026 baada ya kuifunga Aluminium FC kwa mikwaju ya penalti katika mchezo wa fainali.
Mashindano hayo yalianza Juni 14 na kuhitimishwa Julai 10, 2026, yakihusisha timu 16 zilizoshiriki kwa mfumo wa mtoano.
Akizungumza wakati wa hafla ya kufunga mashindano hayo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tarime/Rorya, Marck Njera, alisema lengo la kuanzishwa kwa ligi hiyo ni kushirikisha jamii katika kudumisha amani,mshikamano na ushirikiano katika mapambano dhidi ya uhalifu.
Alisema kaulimbiu ya Ligi ya Polisi Jamii Cup 2026 ilikuwa,"Tarime/Rorya bila uhalifu inawezekana."Kamanda Njera alitumia nafasi hiyo kuwakabidhi mabingwa Tarime All Star zawadi ya ng'ombe iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalumu, Eliakimu Maswi, pamoja na kombe,seti moja ya jezi na mpira wa miguu.
Kamanda Njera alionyesha kukerwa na mila iliyopitwa na wakati ya ukeketaji kuendelea kushikiliwa ambapo alisema kuna haja jamii kutumia mila hiyo kubadikika na kufanya matukio ya milanisiyo kandamizi na ya kikatili ambayo inakubalika kwa jamii.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kituo cha Polisi Tarime, Fatuma Mbwana, alisema mashindano hayo yalifanyika kuanzia Juni 14 hadi Julai 10, 2026, yakishirikisha jumla ya timu 16.
Alisema mshindi wa pili alizawadiwa seti moja ya jezi, mpira mmoja wa miguu na nishani za dhahabu, huku mshindi wa tatu akipata seti moja ya jezi, mpira mmoja wa miguu na nishani kwa kila mchezaji. aidha, kila timu iliyoshiriki ilikabidhiwa mpira wa miguu na nishani, huku waamuzi bora, mchezaji bora na mfungaji bora wa mashindano wakizawadiwa zawadi mbalimbali.
Fatuma alisisitiza kuwa Ligi ya Polisi Jamii Cup itakuwa endelevu na kuwahimiza wadau mbalimbali kuendelea kujitokeza kuunga mkono mashindano hayo kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na jamii.

