Biashara Horohoro–Lungalunga yafikia Sh. bilioni 548.8

 


Na Rebeca Duwe Horohoro


Mwenendo wa biashara kati ya Tanzania na Kenya kupitia Kituo cha Huduma cha Pamoja cha Mpakani cha Horohoro na Lungalunga umeendelea kuimarika, huku thamani ya bidhaa zinazoingia ikiongezeka kutoka Sh. bilioni 306.4 mwaka wa fedha 2022/23 hadi Sh. bilioni 548.8 mwaka 2024/25.


Mafanikio hayo yameelezwa kuwa yanatokana na ushirikiano mzuri kati ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Mapato Kenya (KRA), ambao umeongeza ufanisi wa utoaji wa huduma na kurahisisha biashara ya mipakani.



Akitoa taarifa ya utendaji wa kituo hicho mbele ya Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Bi. Annet Semwamba, wakati wa ziara yake ya kutembelea kituoni hapo, Afisa Mfawidhi wa Kituo cha Huduma cha Pamoja cha Horohoro (OSBP), Shadrack Mbonea Kavuta, alisema katika mwaka wa fedha 2025/26 thamani ya bidhaa zilizoingia imefikia Sh. bilioni 489.5, hali inayoendelea kuashiria uimarikaji wa biashara kati ya nchi hizo mbili.



Kavuta alisema ushirikiano kati ya TRA na KRA umeongeza kasi ya utoaji wa mizigo mpakani, ambapo thamani ya bidhaa zilizosafirishwa nje kupitia kituo hicho imeongezeka kutoka Sh. bilioni 134.7 mwaka 2022/23 hadi Sh. bilioni 175.9 mwaka 2025/26.


"Ongezeko hili linaonyesha kuwa mazingira ya biashara yanaendelea kuboreshwa na wafanyabiashara wanapata huduma kwa ufanisi zaidi kupitia kituo hiki," alisema Kavuta.


Hata hivyo, alisema kituo hicho kinakabiliwa na changamoto za ukosefu wa umeme wa uhakika pamoja na vifaa vya kuzimia moto, hali inayoweza kuhatarisha usalama wa watumishi, wafanyabiashara na mali zinazopita mpakani.


Aliiomba Jumuiya ya Afrika Mashariki kuisaidia Serikali katika kutatua changamoto hizo ili kuongeza ufanisi wa huduma na kuzuia hasara zinazoweza kujitokeza.


Kavuta alisema Kituo cha Huduma cha Pamoja cha Horohoro kinajumuisha taasisi 19 za Serikali zinazofanya kazi kwa pamoja chini ya uratibu wa TRA. Taasisi hizo ni pamoja na Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, TMDA, TAWA, TASAC, Tume ya Madini, TFS, GCLA, Idara ya Mifugo, Idara ya Uvuvi na taasisi nyingine zinazohusika na usimamizi wa biashara na usalama wa mipakani.


Alisema jukumu kuu la kituo hicho ni kukusanya mapato ya Serikali, kurahisisha biashara, kudhibiti magendo, kulinda jamii dhidi ya bidhaa hatarishi, kutekeleza sera na mikataba ya biashara ya kimataifa pamoja na kukusanya na kuhifadhi takwimu za biashara.


Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bi. Annet Semwamba, alisema ameridhishwa na maendeleo yaliyofikiwa katika Kituo cha Huduma cha Pamoja cha Horohoro, akibainisha kuwa ongezeko la biashara linaonyesha mafanikio ya utekelezaji wa mfumo wa vituo vya pamoja vya mipakani katika ukanda wa Afrika Mashariki.


Aliwapongeza watumishi wa kituo hicho kwa kazi nzuri wanayoifanya na kuahidi kuwa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki itashirikiana na mamlaka husika kuhakikisha changamoto zilizowasilishwa zinapatiwa ufumbuzi ili kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi wanachama.


Mwisho

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi