Chirwa: Nitawajibu mechi ya Simba Taifa

UKAME wa mabao, unaomwandama, straika wa Yanga, Mzambia Obrey Chirwa umezusha maswali mengi kwa wadau wa soka kwani tangu asajiliwe ameshindwa kupachika bao hata moja, lakini yeye akasisitiza, atajibu maswali yote baada ya mechi dhidi ya Simba kumalizika.

Chirwa ambaye thamani yake ndani ya kikosi hicho inakadiriwa kuwa ni Dola laki moja ambayo ni sawa na Sh. 200 milioni, akitokea FC Platnum ya Zimbabwe, ameshacheza mechi  za Kombe la Shirikisho dhidi ya TP Mazembe, Bejaia na Medeama na za ligi dhidi ya Ndanda na Majimaji.

Na kutokana na tatizo hilo, wapo wanaomkejeli kuwa ni galasa na hana msaada wowote kwa Yanga, lakini wapo wanaoshangazwa kwa nini hafungi wakati ana sifa zote za kuwa mchezaji.

Akizungumza na Mwanaspoti, Chirwa alisema: “Nitakuwa na la kuzungumza mara baada ya mechi yetu na Simba. Hapo ndipo nitakuwa na majibu yote ya walio na maswali juu yangu kwa sasa wazungumze tu.”

Hata alipoulizwa maana ya kauli hiyo huenda anatarajia kufanya mambo makubwa katika mchezo huo, Chirwa alikazia maneno yake na kusema: “Wewe subiri tu mchezo huo na Simba uishe ndiyo kila kitu kitakuwa wazi.”

Simba na Yanga zinakutana Oktoba Mosi, Uwanja wa Taifa mchezo ambao kwa kawaida huwa na ushindani mkubwa. Kocha wa Yanga, Hans Pluijm alipoulizwa, hakutaka kumzungumzia mchezaji huyo na kwamba muda wake utafika.

Kocha wa timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17, Bakari Shime amesema: “Chirwa aliletwa baada ya kuonekana anafanya vizuri, lakini tatizo lililopo, huko alipotoka alikuwa akitumiwa vipi kulingana na ubora na mchezaji pamoja na mbinu. Anaweza kuwa mchezaji mzuri lakini akakosa bahati.”

“Au thamani ambayo amepewa ndani ya Yanga na akiangalia uwezo wa wachezaji wenzake aliowakuta, inamfanya ajibebeshe mzigo mkubwa ili kulipa deni alilonalo na kushindwa kufanya vizuri.“Kama anaendelea kupata nafasi ndani ya kikosi anaweza kufanya vizuri, yeye ni mchezaji mzuri.”

Mpya zaidi Nzee zaidi