‘Dumisheni amani kipindi hiki cha mwisho wa mwaka’

WATANZANIA wametakiwa kudumisha amani na mshikamano ili kuhakikisha nchi inabaki na amani. Hayo yalisemwa Dar es Salaam na Mufti wa Tanzania, Shehe Abubakar Zubeir, wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Mufti Zubeir alisema kwa kipindi cha mwisho wa mwaka kumekuwa na matukio mbalimbali ya uvunjifu wa amani, lakini ni jukumu la kila Mtanzania kuhakikisha anailinda amani iliyopo kwa kuhakikisha anapambana na viashiria vya uvunjifu awa amani.

“Amani ndio maendeleo na unapozungumzia amani unazungumzia uchumi, usalama, utulivu na kila kitu, hivyo lazima watanzania wote kama tunataka kuwa na yote haya ni lazima nchi iwe na amani na utulivu,” alieleza.

Aliongeza kuwa suala la kulinda amani ni jukumu na kila mtu na kwa dini yoyote na endapo itatokea viashiria vya kuvunja amani, basi kila Mtanzania anapaswa kuvikabili na kuviondosha ili kuhakikisha amani illiyohasisiwa inabaki na nchi inabaki kuwa na amani na utulivu.

Aidha, Mufti Zubeir amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa ujenzi wa Ofisi ya Makao Makuu ya Bakwata Kinondoni na kupongeza juhudi zinazoendelezwa na wafadhili GSM Foundation kwa hatua ya ujenzi wa jengo hilo ulipofikia.

“Hii ni ofisi ya kihistoria tunashukuru sana Mkuu wa Mkoa na GSM tunaamini na wadau wengine wenye mioyo ya kujitolea watajitokeza kusaidia katika sehemu mbalimbali,” alieleza kiongozi huyo wa Waislamu Tanzania.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items