Tarime. Waliokuwa wajumbe wa kikosi kazi cha kutathmini mali za wananchi waishio karibu na mgodi wa North Mara sasa kuchunguzwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorious Luoga alitoa agizo hilo baada ya kuibuka tuhuma za kuwapo orodha ya majina hewa 720 yaliyowasilishwa na kamati hiyo iliyotekeleza kazi mwaka 2014.
Akihutubia mkutano wa hadhara katika Kitongoji cha Nyamichere Kijiji cha Nyakunguru Kata ya Kibasuka wilayani hapa juzi, alisema udanganyifu uliofanywa na wajumbe wa kamati hiyo ulisababisha baadhi ya wananchi kucheleweshewa fidia.
Alisema udanganyifu huo ulibainika baada ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuunda kamati nyingine kupita kila kijiji kuzungumza na wananchi kutafuta chanzo na njia ya kutatua mgogoro wa fidia.
Kamati ya Muhongo ilibaini majina 883 ya wananchi waliostahili fidia pamoja na mengine 720 yaliyokuwapo kwenye orodha ya mgodi lakini hayapo katika orodha iliyohakikiwa na Kijiji cha Nyakunguru.
Katika mkanganyiko huo, Luoga alisema majina 137 yapo kwenye orodha ya Kijiji cha Nyakunguru yaliyowasilishwa serikalini lakini hayamo kwenye orodha ya mgodi.
Alisema baada ya uchunguzi unaotarajiwa kukamilika Januari 20 mwakani, watakaobainika kufanya udanganyifu watachukuliwa hatua za kisheria ili kutoa fundisho kwa wengine.
Baada ya uchunguzi na uhakiki mpya, aliahidi wananchi hao watalipwa stahiki zao pamoja na fidia ya asilimia nane.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyakunguru, Abel Maginga aliwatupia lawama wakazi wa eneo hilo akidai ndiyo walitumia ujanja kuingiza majina kwenye orodha ya tathmini kinyume cha taratibu.
