Utata waizingira Mv Dar es Salaam

Dar es Salaam. Kampuni iliyotengeneza kivuko cha Mv Dar es Salaam imenawa mikono kuhusu chombo hicho, ikisema hakiko mikononi mwake kwani ilishakikabidhi na kupokewa na Wakala wa Umeme, Mitambo na Ufundi (Temesa) ambao ulikitumia kusafirisha abiria.

Pia, kampuni hiyo ya Denmark iitwayo JGH Group (JGH Marine A/S/Johs. Gram-Hanssen A/S) imesema ingawa imekubali kimsingi kukifanyia marekebisho kivuko hicho kwa lengo la kuongeza kasi, “Bado kuna mambo kadhaa yaliyosalia kumaliziwa na kufikiwa mwafaka kabla ya kuanza kazi hiyo.”

Katika barua pepe aliyoandika kwa gazeti hili, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa Kampuni ya JGH Group (JGH Marine A/S / Johs. Gram-Hanssen A/S), Andreas Gottrup alisema si kweli kwamba chombo hicho kiko mikononi mwao kama ilivyodaiwa na Serikali, bali kiko chini ya Temesa.

“JGH tunajiandaa kufanya marekebisho hayo kutokana na uhusiano mzuri tulionao na Serikali ya Tanzania, ingawa kivuko kilikubaliwa na kupokewa. Ndiyo kusema kiko kwenye mikono ya Temesa ambao walikitumia kusafirisha abiria,” alisema Gottrup.

Gottrup, ambaye ofisi zake za kanda ziko Nairobi, Kenya alisema wamekuwa wakizungumza na Temesa na kimsingi wamekubaliana kuifanyia marekebisho ya kuongeza kasi yake lakini, “bado kuna mambo yaliyosalia kumaliziwa na kufikiwa mwafaka kabla ya kuanza kazi hiyo.”

“Temesa wametuomba na tumekubaliana kazi ya marekebisho ifanyiwe Dar es Salaam badala ya nje ya Tanzania. Kuanzia yatakapofikiwa makubaliano ya mwisho na kuendelea na marekebisho hadi kukamilika, tunatarajia kutumia takribani wiki 21 ila hatuwezi kufafanua gharama zitakazotumika, lakini zitakuwa kubwa,” alisema.

Maelezo hayo yanakinzana na ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani aliyeliambia Taifa hivi karibuni kuwa kivuko hicho kiko mikononi mwa mzabuni.

“Kivuko bado kiko kwa mzabuni. Kiko hapahapa Dar es Salaam. Kimeegeshwa kule Navy (Jeshi la Wanamaji) kuna marekebisho anayofanya ya kuongeza kasi ili ifikie tuliyokubaliana kwenye mkataba,” alisema Ngonyani.

“Hatujampa muda maalumu, yeye anataka amalize ili tumlipe na sisi tunataka kivuko. Wakati ule tulimpa deadline (mwisho wa muda) ndipo akatuletea kivuko kibovu. Kama akishindwa basi aondoke na kivuko chake.”

Mwanzo wa utata

Kivuko hicho kilichonunuliwa mwaka 2014 kwa lengo la kurahisisha usafiri kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo, kimeshindwa kufanya kazi kwa mwaka wa pili sasa, huku Serikali ikiwa na maelezo yanayotofautiana.

Mv Dar es Salaam ililetwa nchini Novemba 2014 na kuzinduliwa na aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli (Sasa Rais) na ilitarajiwa kuwa na uwezo wa kubeba abiria 300 waliokaa pamoja na mizigo huku ikiwa inasafiri kwa kasi ya wastani wa kilomita 40 kwa saa.

Hata hivyo, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2014/15 iliyowasilisha bungeni, ilibaini kuwapo kwa upungufu katika taratibu za ununuzi wa kivuko hicho cha Sh7.9 bilioni.

CAG Profesa Mussa Assad alisema Temesa iliingia mkataba na M/s Johs. Gram-Hanssen Bergensgade 10, DK 2100 Copenhagen Oe Denmark wa ununuzi wa kivuko cha Dar es Salaam–Bagamoyo chenye thamani ya Dola za Marekani 4,980,000 bila Kodi ya Ongezeko la thamani (VAT).

“Mapungufu yafuatayo yalibainika katika manunuzi hayo: Kasi ya kivuko haikuzingatia matakwa ya mnunuzi. Ripoti ya mtaalamu wa ukaguzi ilibainisha kwamba kiwango cha juu na chini cha kasi ya kivuko wakati wa majaribio kilikuwa kati ya knots 19.45 na 17.25 kinyume na makubaliano yaliyoainishwa kwenye mkataba ya kasi ya kiwango cha knots 20,” inasema taarifa hiyo.

Profesa Assad alifichua, “Kivuko kilikabidhiwa bila hati ya makabidhiano Novemba 17, 2014 baada ya ucheleweshwaji wa siku 16; pia nilibaini kwamba mpaka wakati wa ukaguzi, Augusti 2015, hati ya makabidhiano ilikuwa haijatolewa na mzabuni kinyume na kanuni ya 248 ya mwaka 2013 ya manunuzi ya umma.”

Kutokana na upungufu huo, CAG alipendekeza katika ripoti hiyo kuwa Temesa iwasiliane na mzabuni kufanya marekebisho ya upungufu wote uliobainishwa kwenye kivuko hicho na pia hati ya makabidhiano itolewe kulingana na kanuni ya ununuzi wa umma ya mwaka 2013.

Lakini katika Bunge la Aprili mwaka huu, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alipinga kukiukwa kwa kanuni za ununuzi kama ilivyoelezwa na CAG.

“Ni kweli kivuko kina mapungufu ikiwamo kasi ndogo, lakini hakuna ukiukwaji wowote wa taratibu wakati wa ununuzi. Temesa ilitangaza zabuni na baada ya maombi kupitiwa, kampuni ya MS Jones Gram Hansen ilishinda zabuni hiyo kwa kuwa na bei nafuu,” alisema Profesa Mbarawa.

Waziri huyo aliwaambia wabunge kuwa baada ya kivuko kuletwa nchini Desemba 2014, kilifanyiwa majaribio na kubainika kwamba hakikuwa na kasi ya kuridhisha na kwamba makubaliano yalikuwa ya kujenga kivuko chenye kasi ya knots 20, lakini hicho kilikuwa na kasi ya knots 15.7.

Profesa Mbarawa alisema kutokana na hali hiyo, Serikali ilimtaka mkandarasi kurekebisha kasoro hiyo kwa gharama zake na kuwa ameshawasilisha andiko juu ya namna atakavyoifanya kazi hiyo.

“Mpaka sasa mzabuni huyo hajalipwa asilimia 10 ya malipo yaliyokubaliwa mpaka pale atakapokamilisha kazi hiyo. Kwa hiyo, taratibu zote zilifanyika kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Mapema mwezi uliopita, Mwananchi ilimfuata Profesa Mbarawa afafanue kuhusu hatima ya kivuko hicho, lakini alimtaka mwandishi kumuuliza Ofisa Mtendaji Mkuu wa Temesa, Dk Musa Mgwatu.

Alipofuatwa Dk Mgwatu ambaye aliteuliwa Septemba 19 kuchukua nafasi ya Mhandisi Marcellin Magesa aliyepangiwa majukumu mengine, alitaka apelekewe maswali ofisini lakini takwa hilo lilipotekelezwa maswali hayo hayakujibiwa.

Wiki mbili baadaye alimwambia mwandishi kuwa maswali hayo yameshajibiwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Edwin Ngonyani. “Maswali yako yameshajibiwa na Naibu Waziri, nilijua tu utaniuliza. Wewe si ni mwandishi? Fanya kazi yako ujue aliongelea wapi,” alisema Dk Mgwatu.

Novemba 21 mwaka huu, Waziri Ngonyani alikaririwa na gazeti moja la kila siku akitoa kauli iliyoonekana ni kujibu ripoti ya CAG akisema, “Hatukukipokea kivuko hicho tulimrudishia mzabuni arekebishe kasoro hizo kwanza, kwa hiyo kwa sasa kivuko hakiko mikononi kwetu, na kikishindwa kabisa kufikia viwango vyetu tulivyowekeana hatutakipokea.”

Ingawa Ngonyani alidai “kikishindwa kufikia viwango vyetu tulivyowekeana hatutakipokea,” pia alisema Serikali inaangalia uwezekano wa kupeleka kivuko hicho kikafanye safari kati ya kisiwa cha Mafia na Nyamisati wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items