Wanne washambuliwa kwa imani za kishirikina

WANAWAKE wanne wakazi wa Kijiji cha Kihumbu Wilaya ya Bunda mkoani Mara, wamejeruhiwa vibaya baada ya kushambuliwa na waombolezaji wakituhumiwa kuhusika na ifo cha mwanafunzi mkazi wa kijijini hapo.

Majeruhi hao ambao walishambuliwa kwa silaha za jadi zikiwamo fimbo, marungu na vitu vizito, kwa sasa wamelazwa katika Hospitali Teule ya wilaya hiyo (DDH) wakiendelea na matibabu.

Mwanafunzi anayedaiwa kuuawa kimazingara na wanawake hao, alikuwa akitibiwa kwa mganga wa jadi.

Tukio hilo lilitokea juzi majira ya mchana katika Kijiji cha Kihumbu Kata ya Hunyari wilayani hapa.

Ilidaiwa kuwa baada ya mtoto huyo, Waryo Mseti (12), aliyekuwa akisoma darasa la nne katika Shule ya Msingi Kihumbu, kufariki dunia, wazazi wake walikwenda kwa mganga wa jadi kupiga ramli wakiamini kwamba kifo chake si cha kawaida.

Inadaiwa kuwa mganga huyo wa jadi aliwaeleza kuwa mtoto huyo alirigwa na wanawake hao.

Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Chacha Warioba, alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo.

Ilielezwa kuwa baadhi ya wananchi na waombolezaji baada ya kupata taarifa hizo, walianza kuwasaka wanawake wanaotuhumiwa kwa uchawi huo na kumshika mmoja baada ya mwingine na kuwapeleka mlimani wakiwa wamewafungwa kamba huku wakiwatishia kuwachinja wakiwataka wamrudishe mtoto huyo aliyefariki dunia huku wakiwapa kipigo kikali.

Wanawake waliojeruhiwa katika tukio hilo wametajwa kuwa ni Konzira Matiku (58), Nyandumbo Nyambere (78), Malongo Joseph (36) na Mgisi Higosi (44), wakazi wa Kijiji cha Kihumbu.

Aidha, mbali ya wanawake hao kushambuliwa na waombolezaji, imeelezwa kuwa nyumba ya mmoja wa watuhumiwa hao ilimwagiwa mafuta ili iteketezwe kwa moto.

“Walitupiga sana kwa fimbo na silaha nyingine wakitulazimisha eti tumrudishe mtoto huyo waliyedai tulimuua sisi," alisema mmoja wa wanawake hao.

Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Ramadhani Ng’anzi, alithibitisha kwa njia ya simu kuwapo kwa tukio hilo na kusema kuwa wote waliohusika kwa kujichukulia sheria mkononi, lazima watakamatwa na kufikishwa mahakamani.

“Tuliona kwanza tuwaokoe hao watu kwa kuwachukua hadi hospitalini na baadaye tutawasaka wote waliohusika, hakuna kuogopa mtu wala cheo chake,” alisisitiza Kamanda Ng'anzi.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items

Kilimo cha Bamia