MAKAMU MWENYEKITI WA LAAC, ABDALLAH CHIKOTA.
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), imeagiza mkandarasi aliyejenga nyumba tano za watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, atafutwe na kuzifanyia ukarabati haraka baada ya kubaini nyumba hizo zinavuja na ziko chini ya kiwango.
Kamati hiyo ilitoa agizo hilo juzi muda mfupi baada ya kutembelea mradi wa nyumba za watumishi wa halmashauri hiyo zilizojengwa kwa Sh. milioni 285.
Licha ya kukamilika ujenzi wake, nyumba hizo zimebainika kuwa na dosari nyingi ikiwamo baadhi ya kuta kuwa na nyufa na kuvuja paa kabla hazijaanza kutumika.
Makamu Mwenyekiti wa LAAC, Abdallah Chikota, baada ya ukaguzi huo, alitoa agizo hilo na kusema inashangaza kuona kiasi kikubwa cha fedha kimetumika, lakini nyumba zimejengwa chini ya kiwango na kamati yake haiwezi kukubaliana na hilo.
"Atafutwe mkandarasi aliyejenga nyumba hizi chini ya kiwango, azikarabati haraka iwezekanavyo... Serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo, lakini inasikitisha kuona baadhi ya watu wanachezea fedha hizo na kusababisha miradi kuwa mibovu," alisema Chikota.
Pia aliwataka watumishi wa halmashauri kuwa na umoja katika kusimamia miradi ya maendeleo na iwapo hawatazingatia hilo, mtindo wa uchakachuaji wa miradi ya maendeleo kwa kujenga chini ya kiwango utaendelea.
"Naomba mfanye utaratibu wa kumtafuta mkandarasi aliyejenga nyumba hizi ili arudi azifanyie ukarabati kwani kama nilivyosema, Kamati imejiridhisha kwamba zimejengwa chini ya kiwango, hali hii haikubaliki,'' alisisitiza Chikota.
Makamu Mwenyekiti huyo alimtupia lawama Mhandisi wa Halmashauri wa wilaya hiyo, Wilfred Gutta, kwamba alishindwa kusimamia mradi wa nyumba hizo na kusababisha zijengwe chini ya kiwango.
Taarifa ya mradi wa nyumba iliyotolewa katika ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo, ilionyesha kuwa Sh. milioni 300 zilitengwa kwa ajili ya kujenga nyumba tano za watumishi.
Hata hivyo, ujenzi wa nyumba hizo umetumia Sh. milioni 285 na kubaki Sh. milioni 15.
Ukaguzi huo ulikuwa ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 11 ya maendeleo katika kipindi cha mwaka 2014/2015 na ikabainika kuwa hali ya utekelezaji wake haikuwa nzuri kutokana na nyumba hizo kujengwa chini ya kiwango huku fedha nyingi zikiwa zimetumika.
Kwa upande wake, Mkandarasi Amir Abass, alikiri kasoro katika nyumba hizo na hasa kwenye baadhi ya milango kwamba haifungi na kuahidi kuyafanyia kazi haraka iwezekanavyo.
Pia mkandarasi huyo alifafanua kuwa alijenga kwa gharama ndogo ya Sh. milioni 63 kwa kila nyumba.
"Nimejitahidi sana kujenga kwa gharama ndogo, kwani kwa kawaida nyumba moja ya aina hiyo hujengwa kwa zaidi ya Sh. milioni 100...sisi ni mafundi na tunakiri kwamba katika ujenzi zinaweza kutokea kasoro, ndiyo maana nikasema kuwa tutazifanyia marekebisho," alisema Abass.
Mkandarasi huyo alisema kuwa ujenzi wa nyumba hizo ulianza mwaka 2013 hadi 2014, lakini walisimama na kuendelea tena kwa vile walikuwa wakijenga kwa awamu.
JIUNGE NASI KATIKA
YOUTUBE @Muungwana Tube
BOFYA HAPA KU-INSTALLAPP YA MUUNGWANA BLOG ILI UPATE URAHISI KUZISOMA HABARI ZOTE KWA WAKATI.