Huduma za mawasiliano vijijini Wasiofika maeneo waliyoomba leseni kunyang’anywa

Serikali imetishia kuzinyang’anya leseni za masafa kampuni za huduma za mawasiliano nchini zilizopewa ruzuku ya kutekeleza miradi ya kufikisha huduma za mawasiliano vijijini lakini yameshindwa kukamilisha miradi hiyo.

Serikali kupitia mfuko wa Mawasiliano kwa wote, imekuwa ikitoa ruzuku ya fedha za ujenzi wa minara ya mawasiliano kwenye kata 443 zilizopo maeneo ya vijijini ili kufikisha huduma ya mawasiliano ya simu lakini hadi sasa ni kata 322 pekee zilizofikiwa na makampuni yaliyotakiwa kutekeleza miradi hiyo.

Kampuni za Airtel, MIC inayoendesha Mtandao wa Tigo, Vodacom Tanzania na TTCL kwa pamoja yamedaiwa kutokamilisha miradi ya kufikisha huduma za mawasiliano ya Simu Vijijini kwenye Kata 121 hapa nchini.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof MAKAME MBARAWA ameutaka mfuko wa Mawasiliano kwa wote kuhakikisha unazifuatilia kwa karibu kampuni hizo ili ziweze kukamilisha miradi hiyo, ambayo kwa mujibu wa makubaliano inatakiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.

Katika Hatua nyingine, Waziri Mbarawa ameutaka uongozi wa kampuni ya Simu Tanzania TTCL, kuwa na mipango bunifu itakayosaidia kuongeza idadi ya wateja, sambamba na kupunguza idadi ya watumishi wanaobaki maofisini badala ya kwenda mitaani kutafuta wateja.

JIUNGE NASI 
 INSTA@MUUNGWANABLOG ,FB@MUUNGWANABLOG,YOUTUBE @MUUNGWANA TUBE, BOFYA HAPA KU-INSTALL APP YA MUUNGWANA BLOG ILI UPATE URAHISI KUZISOMA HABARI ZOTE KWA WAKATI.
Mpya zaidi Nzee zaidi