
Geita\Dar. Vilio na simanzi vimetawala katika eneo la Mgodi wa RZ uliopo Nyarugusu wilayani Geita, wakati shughuli za uokoaji wa wachimbaji 14 waliofukiwa na kifusi cha udongo usiku wa kuamkia Januari 26, zikiendelea.
Wakiwa pembezoni mwa eneo la mgodi baadhi ya ndugu wameshindwa kujizuia na kuanza kulia baada ya kuona mitambo ya uokozi ikiendelea kufukua udongo.
Zilikuwa zimepita zaidi ya saa 40 mpaka jana, wachimbaji hao wakiwa bado umbali wa mita zaidi ya 35 kwenda chini ya ardhi.
Akizungumza na gazeti hili huku akibubujikwa na machozi, Neema Charles, ambaye ni miongoni mwa watu ambao ndugu zao wamefukiwa alisema katika mgodi huo yumo mumewe aliyemtaja kwa jina la Amani Masikiti.
Alisema aliagana na mumewe Januari 25 majira ya saa mbili usiku na aliamini angerudi asubuhi ya siku inayofuata, lakini hakumuona hadi alipopata taarifa ya kufukiwa juzi mchana.
“Mume wangu alishinda nyumbani tukala chakula cha usiku kisha akaaga kwenda kazini maana alikuwa anaingia zamu ya usiku. Asubuhi alichelewa kurudi, lakini sikujali ila ilipofika saa nne nikaanza kuogopa, baadaye nikaamua kutoka nyumbani ndipo nikakutana na wachimbaji wenzake wakaniambia amefukiwa na kifusi,” alisema.
Neema ambaye ni mama wa mtoto mmoja alisema hawezi kueleza zaidi kwa kuwa maisha yake na mwanaye wanamtegemea baba huyo ambaye amefukiwa na kusema zaidi wanamuomba Mungu waliofukiwa waokolewe wakiwa salama.
Sabina Magidinga alisema katika mgodi huo amefukiwa mtoto wake ambaye ameanza shughuli za uchimbaji mwaka huu na kuomba Mungu amlinde ili atoke salama.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Ezekiel Kyunga ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama alisema bado shughuli za uokozi zinaendelea na lengo ni kuwatoa wachimbaji hao wakiwa hai.
Alisema mpaka sasa chanzo cha ajali hakijafahamika na kuwa pamoja na miti (matimba) iliyokuwa ikishikilia udongo kuonekana imeoza, hawawezi kusema kuwa ndiyo chanzo na kuwataka wataalamu wa migodi wanapopita kufanya ukaguzi kuwa makini zaidi ili kuepuka ajali zisizo za lazima.
“Wataalamu wetu watafanya uchunguzi na ndiyo watakuja na majibu sahihi ya nini kimesababisha ajali. Hatuwezi kutoa uamuzi kwa sababu tumeona matimba yameoza. Hatuwezi kusema hayo ndiyo sababu, tusiishi kwa hisia tusubiri uchunguzi utatupa kioo cha kufuatilia kwenye migodi mingine ili kuzuia ajali,” alisema.
Pia, aliwataka wananchi na ndugu kuvumilia wataalamu wafanye kazi zao kwa kuwa tayari mitambo ya kutosha ipo.
Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Ziwa Magharibi, Yahya Semamba alisema tayari wamechimba mita 20 kwenda chini na shimo linasadikiwa kuwa na mita 35 na kwamba, lengo lao ni kuzunguka shimo hilo ili kuepuka udongo kutitia tena.
Rais wa Shirikisho la Wachimbaji Madini nchini, John Wambura alipongeza jitihada za Serikali na kampuni binafsi za madini zilivyoonyesha ushirikiano katika uokozi na kuwaasa wachimbaji kufanya shughuli zao kisasa ili kuepuka ajali zisizo za lazima.