Polisi wazuia wafanyakazi kuandamana

POLISI wamezima maandamano ya Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) yaliyotaka kufanyika kwenda ofisini kwa Waziri Mkuu.

Talgwu walitaka kuandamana mjini hapa jana ili kwenda kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwasilisha kilio chao kutokana na jengo la kitega uchumi chao kuzuiwa kuendelea kujengwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akidai linajengwa chini ya viwango.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa amethibitisha kwamba viongozi wa chama hicho walikwenda kuomba kibali cha kufanya maandamano ili kumwona Waziri Mkuu, lakini walikataliwa kutokana na jeshi la polisi halikuwa na uwezo wa kulinda maandamano hayo kutokana na kuwepo kwa shughuli za kibunge.

Kutokana na kukataliwa kuendelea kujenga kitegauchumi hicho, viongozi wa chama hicho wakiongozwa na Katibu Mkuu wao Taifa, Rashidi Mtima walitaka kufanya maandamano lakini polisi waliyazuia kabla hawajaanza kuandamana kutoka katika ukumbi wa mikutano ya Royal Village mjini hapa.

Akitoa malalamiko yake mbele ya waandishi wa habari kabla ya Polisi kufika na kutawanya kusanyiko hilo, Katibu Mtima alisema Makonda amekuwa kikwazo kwa kuzuia ujenzi wa jengo lao la kitega uchumi lililopo Temeke, Dar es Salaam.

Amesema kitendo hicho cha kuzuia ujenzi wa jengo hilo kwa madai kuwa jengo hilo halina ubora na kuagiza mamlaka zinazohusika zifanye ukaguzi wa jengo hilo, ndiko kulikowafanya waje kuomba msaada wa Waziri Mkuu.

Amesema Makonda alitoa amri ya kuzuia ujenzi wa jengo hilo Mei 21, mwaka jana na ilipofika Julai mwaka jana, chama hicho kilikamilisha taratibu zote, lakini mpaka sasa hakuna jibu lolote na badala yake wanadai amekuwa akijificha na hakutani na viongozi wa chama hicho.

Mpya zaidi Nzee zaidi