Simba: Tutakufa na Azam

Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja.

KOCHA Msaidizi wa timu ya soka ya Simba, Jackson Mayanja amesema baada ya kutoka suluhu ya bila kufungana na Mtibwa Sugar katika mechi ya Ligi Kuu juzi, nguvu zote sasa zinaelekezwa kuikabili Azam kwenye mchezo wao wa Januari 28.

Mayanja, alisema hayo juzi baada ya kumalizika kwa mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri mjini hapa, ambapo matokeo hayo ya sare ya bila kufungana yameifanya Simba iongoze ligi kwa tofauti ya pointi mbili kutoka nne za awali.

“Mchezo haukuwa mbaya, wachezaji wamecheza vizuri, lakini hawakuweza kupata magoli licha ya kupata nafasi zaidi ya mbili za kuwezesha kupata ushindi,” alisema Mayanja.

“Tumemaliza mchezo wetu na Mtibwa Sugar na kuambulia pointi moja, na sasa tunaelekeza nguvu kwenye mchezo wetu na Azam… huko tunajiandaa na ushindi,” alisema Mayanja.

Mayanja alisema baada ya mchezo huo wanajipanga kufanya mazoezi kwa ajili ya kukabiliana na Azam, na kutabiri kuwa mchezo huo utakuwa mgumu kulingana na historia ilivyo kwa timu hizo kwa siku za hivi karibuni zinapokutana.

“Siwezi kuizungumzia sana Azam kwavile mechi hiyo bado lakini tunajipanga vizuri kuikabili kwenye mchezo huo,” alisema Mayanja.

Simba ilikutana na Azam kwenye fainali za Kombe la Mapinduzi Zanzibar hivi karibuni na kulala kwa bao 1-0, matokeo yanayotabiri ugumu wa mechi ya marudiano ya timu hizo. Katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Simba ilishinda.

Aidha, Mayanja alisema kupata ushindi ugenini ni jambo gumu na linachangiwa na sababu mbalimbali hivyo wanajiandaa kukabili michezo za ugenini katika michezo ijayo. Pamoja na hayo, aliisifu Mtibwa Sugar kwa kucheza vyema katika mchezo huo tofauti na iliyokuwa mchezo wao wa kwanza uliofanyika Jijini Dar es Salaam.

Naye kocha msaidizi wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila amewasifu wachezaji, benchi la ufundi na uongozi wa timu hiyo kwa kuonesha ushirikiano uliowezesha kupata sare dhidi ya Simba.

Katwila ambaye ni mchezaji wa zamani wa Mtibwa Sugar kwa sasa amekabidhiwa timu hiyo baada ya kocha wake mkuu Salum Mayanga kupewa mikoba ya timu ya taifa, Taifa Stars.

Alisema, mafanikio ya timu yoyote ile ikiwemo ya Mtibwa Sugar yanachangiwa na kuwepo mashabiki wanaoiunga mkono katika kila jambo liwe la mafanikio ya ushindi, sare na hata pale inapopoteza mchezo.

“Vijana wamepigana kufa kupona, tumepata pointi moja kwenye mchezo mgumu ambao washindani wetu wakiwa wametokea kwenye mashindano ya Kombe la Mapinduzi wamekuwa pamoja kimchezo,” alisema Katwila.



JIUNGE NASI KATIKA
INSTAGRAM @Muungwanablog

FACEBOOK @Muungwana Blog

YOUTUBE @Muungwana Tube

BOFYA HAPA KU-INSTALLAPP YA MUUNGWANA BLOG ILI UPATE URAHISI KUZISOMA HABARI ZOTE KWA WAKATI.

Mpya zaidi Nzee zaidi