Wabadili majina kuikwepa TRA

MWENYEKITI WA KAMPUNI YA UDALALI YA YONO AUCTION MART, STANLEY KEVELA.

BAADHI ya wafanyabiashara wanaotafutwa kwa tuhuma za kutorosha kontena 329 bila kulipiwa kodi, wamebadili majina ya biashara zao ili kukwepa kukamatwa.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kampuni ya Udalali ya Yono Auction Mart, Stanley Kevela, wakati akizungumzia maendeleo ya operesheni ya kuwasaka waliotorosha makontena ambayo yalikuwa hayajalipiwa kodi.

Alisema katika operesheni inayoendelea, juzi walifunga duka la mfanyabiashara mmoja lililoko Mtaa wa Sikukuu, Kariakoo, jijini Dar es Salaam ambaye anadaiwa kodi ya Sh. milioni 28.2 na Mamlaka ya Mapato (TRA).

Wafanyabiashara waliotorosha kontena hizo 329 waliisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 18, na kampuni ya Yono ilipewa kazi na TRA kuwatafuta na kuwafilisi ili kufidia kodi hiyo ya serikali wanayodaiwa.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Yono, wamefanikiwa kurejesha TRA Sh. bilioni saba, huku wakiendelea kukamata mali za wadaiwa kufidia kiasi cha Sh. bilioni 11.4 kilichobaki.

Kevela alisema baadhi ya wadaiwa wamebadili namba ya utambulisho ya mlipa kodi (Tin), namba za simu za mkononi na majina ya fremu za maduka ili kukwepa kukamatwa kwenye msako unaoendelea.

“Mbinu zote hizo tumezibaini na sisi tumejipanga vizuri kuhakikisha serikali inapata kodi yake, wajitokeze walipe tu maana mwisho wa siku watakamatwa na kufilisiwa,” alisema.

Kevela alisema kuna wafanyabiashara ambao walijitokeza na kuandikisha mkataba wa kuendelea kulipa kidogo kidogo hadi watakapomaliza kodi wanayodaiwa na TRA.

“Kuna wafanyabiashara wazalendo ambao wameandika mkataba wa kulipa kidogo kidogo na wengine wameshamaliza, lakini hawa wanaojidanganya kubadili badili majina ya biashara ili kutukwepa wajue siku zao zinahesabika na watakamatwa tu,” alisema Kevela.

Muda mfupi tangu kuanza kwa awamu ya tano ya serikali Novemba 2015, Waziri Mkuu Kassim alifanya ziara ya kushtukiza kwenye Bandari ya Dar es Salaam na kufichua utoroshaji wa makontena hayo zaidi ya 300 kupitia bandari kavu (ICD) katika kipindi cha miezi minne ya mwaka 2014.

Kufuatia ugunduzi huo, wiki mbili baadaye TRA ilitaja majina ya kampuni 43 na wamiliki wa makontena 329 ambayo yalipitishwa bandarini bila kulipiwa na kufichuliwa na Majaliwa.

TRA ilisema kwa ujumla, kampuni hizo zilipitisha makontena hayo yaliyoondolewa kinyume cha taratibu kutoka ICD ya Azam inayomilikiwa na kampuni ya Said Salim Bakhresa And Company Limited.

Mamlaka hiyo ilisema bidhaa zilizokuwamo ndani ya makontena hayo ni pamoja na matairi ya magari, samani mbalimbali, betri za magari, vifaa vya ujenzi, nguo na bidhaa zingine mchanganyiko.

Source: Nipashe

JIUNGE NASI 
 INSTA@MUUNGWANABLOG ,FB@MUUNGWANABLOG,YOUTUBE @MUUNGWANA TUBE, BOFYA HAPA KU-INSTALL APP YA MUUNGWANA BLOG ILI UPATE URAHISI KUZISOMA HABARI ZOTE KWA WAKATI.


Mpya zaidi Nzee zaidi