Wadakwa na kadi bandia za chanjo homa ya manjano

Dar es Salaam. Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imewakamata watu saba kwa kutengeneza kadi bandia za chanjo ya homa ya manjano wakiwa maeneo ya Hospitali ya Mnazi Mmoja.

Kamanda wa kanda hiyo, Simon Sirro alisema Januari 16 majira ya saa tano asubuhi kwenye eneo la Hospitali ya Mnazi Mmoja walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao wakiuza kadi hizo kwa watu wanaofika kupata huduma ya chanjo kabla ya kusafiri kwenda nje ya nchi.

Alisema awali mtoa taarifa alifika hospitalini hapo na kutakiwa kutoa fedha na mmoja wa watuhumiwa hao ili aweze kupatiwa kadi hiyo.

Sirro alisema watuhumiwa waliokamatwa ni walinzi watatu wa hospitali hiyo, mhamasishaji, mjasiriamali, mfanyabiashara na fundi umeme.

Mkazi wa Vingunguti, Alex Ismail alisema mchezo huo umeanza muda mrefu katika hospitali hiyo na kwamba ‘huduma’ hiyo imekuwa ikitolewa kwa malipo ya Sh10,000.
Mpya zaidi Nzee zaidi