
Serikali mkoani Kigoma, imeamua kutoyateketeza mazao ya kilimo yaliyolimwa na wananchi katika hifadhi ya msitu wa Makere kusini kata ya Kagerankanda wilayani Kasulu hadi pale yatakapovunwa na kuweka mikakati mipya ya kuhifadhi msitu huo.
Mkuu wa mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga amesema pamoja na hifadhi hiyo kuvamiwa na kuwepo kwa uharibifu mkubwa unaofikia karibu asilimia hamsini ya msitu, serikali imeweka mikakati mipya ya kukabiliana na wavamizi ambapo sasa wananchi waliolima wataachwa wavune mazao yao na kisha hakuna mwananchi atakayeruhusiwa kuendelea na shughuli zozote ndani ya msitu huo.
Akizungumzia hatua hiyo katibu mwenezi wa CCM wilaya ya Kasulu Masudi Kitowe ameiomba serikali kufanyia kazi maombi ya wananchi juu ya kupewa sehemu ya eneo la hifadhi kutokana na wilaya hiyo kuwa na uhaba wa ardhi ya kilimo huku baadhi ya wakulima wakieleza kuwa kilimo bora kwa kufuata maelekezo ya kitaalam kitasaidia wananchi kutovamia maeneo yaliyohifadhiwa.
Msitu wa hifadhi wa Makere kusini katika kata ya Kagerankanda wilayani Kasulu una ukubwa wa hekta elfu 75 lakini karibu nusu ya msitu huo umevamiwa na wananchi ambao wanaendesha shughuli za kilimo, uchomaji mkaa na ukataji miti katikati ya msitu na hivyo kuuweka hatarini kutoweka.