Waziri Mbarawa ameahidi kubadilisha uongozi wa ngazi ya juu wa shirika la posta Tanzania baada ya kubaini hili

Waziri wa ujenzi, uchukuzi na mawasiliano Prof. Makame Mbarawa ameahidi kubadilisha uongozi wa ngazi ya juu wa shirika la posta Tanzania baada ya kubaini kwamba uongozi uliopo umeshindwa kulipeleka shirika hilo mbele.

Prof. Mbarawa ametoa kauli hiyo baada ya kutembelea shirika hilo alilojitaja kuwa lina raslimali nyingi ambazo zimeshindwa kutumika ipasavyo kutokana na kukosa uongozi ulio imara licha ya kuwa na raslimali watu ya kutosha.

Amesema serikali haitasita kutafuta mtu hata ikibidi kutoka nje ya shirika hilo kama ambavyo imefanya kwa mashirika mengine yaliyokuwa katika hali mbaya likiwemo shirika la reli Tanzania ambalo sasa limeanza kufanya vizuri.

Amebainisha kuwa katika maeneo aliyotembelea amebaini kuwa hata idadi ya wateja ni ndogo ikilinganishwa na huduma zinazotolewa lakini jambo la lililomshangaza zaidi ni kwa baadhi ya wakuu wa idara kushindwa kufahamu hata idadi ya wateja wanaowahudumia kwa siku.

Wakitoa malalamiko yao kwa waziri Mbarawa, baadhi ya wafanyakazi wa shirika hilo wamekiri kuwepo kwa uzembe katika utekelezaji wa majukumu ya viongozi wakitolea mfano kuharibika kwa magari ya kusafirishia mizigo bila kufanyiwa matengenezo na kufikia hatua ya kutumia magari ya kukodi kwa gharama kubwa.
Mpya zaidi Nzee zaidi