Julio: Daraja la Kwanza limekosa heshima

Kocha zamani wa Mwadui, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ amelitaka Shirikisho la Soka Tanzania(TFF) kuitengenezea utaratibu Ligi Daraja la Kwanza kwani imekuwa ni ligi ya isiyoeleweka.

Akizungumza na Mwananchi, Julio alisema imekuwa kama ligi ya mtu au kikundi cha watu maana wanapanga mwamuzi wao, matokeo yanakuwapo tayari na inayoumizwa ni timu isiyotakiwa.

“Yaani Ligi Daraja la Kwanza ni kama ligi yenye faida ya watu fulani, mtu anahakikisha timu fulani lazima ipande kwa sababu anafaidika nayo, ni ligi ambayo haina heshima tena,” alisema Julio ambaye alisusa Mwadui kwa kile alichosema waamuzi wanachezesha na matokeo mkononi.

Hata hivyo, Julio aliipa tano timu ya Lipuli ya Iringa kwa kupanda Ligi Kuu Bara na kuionya kuachana kabisa na siasa ili isije ikarudi mapema walikotoka.

Julio ambaye ni mwenyeji wa mkoa wa Iringa inapotoka timu hiyo, alisema timu nyingi huwa zinaathiriwa kwa kuingizwa siasa ndani yake, hivyo kuchangia kutofanya vizuri.

“Ninawapongeza kwa kuwa timu ya kwanza mwaka huu kupanda daraja kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao, hivyo wanachotakiwa ni kuzidi kushikamana na kuhakikisha wanafanya vizuri mechi zao za ligi wasije kupotezwa na kurudi walikotoka.

“Waifanye Lipuli iwe timu ya mkoa na sio ya chama fulani maana timu nyingi huwa zinapotea mapema kwa kuingiza saisa mara utasikia hii timu ya Chadema mara CCM, kila mtu anajifanya anajua wakiingia huko wamekwisha,” alisema.
Mpya zaidi Nzee zaidi