Lyon yaishika pabaya Simba

Dar es Salaam. Mkono wa mwenyekiti wa zamani wa Simba, Ismail Aden Rage umeshikilia kisu cha kuamua hatima ya Simba dhidi ya African Lyon katika mechi ya Kombe la Shirikisho leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mchezo huo wa raundi ya sita ya kombe hilo, unatarajia kuwakutanisha wachezaji nane waliowahi kucheza pamoja katika kikosi cha Simba B, kabla ya kupandishwa 2013, ukiwa ni mpango ulioanzishwa na Alhaji Rage kwa lengo la kutengeneza wachezaji watakaocheza katika kikosi cha wakubwa siku za usoni.

Wachezaji hao ni Hamad Tajiri, Omar Salum, Miraji Adam, Ramadhan Kipalamoto na Hassan Isihaka wanaochezea African Lyon, wakati kwa Said Ndemla, Jonas Mkude na Ibrahim Ajib wakiwa bado Simba.

Hata hivyo, nyota wengi waliokuwa sehemu ya mwanzo ya mpango huo, hawapo kwenye kikosi cha Simba hivi sasa, ikiwamo nyota hao watano wa Lyon watakaocheza dhidi ya Simba.

Ni wazi uwapo wa nyota hao utaongeza ugumu kwenye mechi hiyo, ambayo inaweza kufufua au kuzika ndoto za Simba kutwaa vikombe viwili vikubwa msimu huu ikiwamo Ligi Kuu baada ya kushindwa kufanya hivyo kwa misimu minne mfululizo.

Rage alisema anajivunia kuona mkakati aliouanzisha matunda yake yanaonekana na kuwa tegemeo kwa timu mbalimbali nchini.

“Binafsi nafurahi kuona vijana hawa wanafanya vizuri na vipaji vyao vimeimarika, kiasi ambacho wamekuwa tegemeo kwa sasa. “Natoa wito kwa viongozi wa timu zetu kuwa soka halina njia za mkato. Waanzishe na kuzisimamia timu za vijana ili waweze kuvuna matunda kama ilivyo kwa vijana hao,” alisema Rage.

Kuimarika kwa safu ya ushambuliaji ya Simba katika siku za hivi karibuni baada ya washambuliaji wake kufunga mabao sita katika mechi mbili zilizopita, huenda kukawa mlima mrefu kwa safu dhaifu ya ulinzi ya Lyon, ambayo imeruhusu mabao saba katika mechi tatu za mwisho za Ligi Kuu.

Hata hivyo, Simba inapaswa kuingia kwenye mchezo wa leo ikiwa na tahadhari hasa na mbinu ya mashambulizi ya kushtukiza, ambayo imekuwa ikitumiwa na Lyon pindi inapocheza mechi na timu kubwa.

Lyon wamekuwa tishio katika kutumia mbinu hiyo kupitia washambuliaji wake, Venance Ludovick, Rehani Kibingu na Abdallah Mguhi na ikumbukwe pia ndiyo ilitumika pindi timu hiyo ilipoifunga Simba bao 1-0 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu. Nyingine ni ‘kupaki’ basi.

Simba itawakosa mabeki wake Abdi Banda na Method Mwanjali, ambao ni majeruhi, ingawa benchi la ufundi limesisitiza kuwa wamejipanga kupata ushindi dhidi ya Lyon.

“Vijana wamefanya maandalizi mazuri kwa ajili ya mchezo na kila mmoja ana morali ya juu kuelekea mchezo huo. Ni mechi ngumu kwa sababu timu zote zilizofika hatua hiyo zimefanya kazi ya ziada, lakini tutahakikisha tunaibuka na ushindi,” alisema Kocha Msaidizi, Jackson Mayanja.
napozaliwa’

Mpya zaidi Nzee zaidi