Ndanda, Mbao, Majimaji, Lyon, Mtibwa, Ruvu, Azam Hapatoshi leo


Ligi Kuu Bara inaendelea leo ikihusisha zaidi timu zilizo katika nafasi mbaya ya kushuka daraja, ambazo zinasaka matokeo kwa hali yoyote ili kuzidi kujinusuru zisiende na maji.

Ndanda iliyo nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 23, inaikabili African Lyon yenye pointi 22 kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara, wakati Mtibwa Sugar ikiikaribisha JKT Ruvu inayoshika mkia ikiwa na pointi 19. Mchezo huo utafanyika kwenye Uwanja wa Manungu, Morogoro.

Majimaji iliyo nafasi ya 15 na pointi 21, itakuwa ugenini kukabiliana na Mbao yenye pointi 26, mchezo utakaofanyika Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, wakati Azam FC itacheza na Mwadui kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam.

Timu 10 kwenye msimamo wa ligi zipo katika hatari ya kushuka daraja wakati michezo saba ikibaki kila moja ikihangaika kujinasua na janga hilo.

Timu za JKT Ruvu, Majimaji, Toto Africans,African Lyon, Ndanda,Mbao, Stand United, Ruvu Shooting, Mbeya City na Prisons zote haziko salama na atakayechanga karata zake vizuri atabaki.

Kocha wa Mbao, Ettiene Ndayiragije licha ya kulalamikia ratiba ngumu inayowachosha wachezaji wake lakini ametamba kukomaa katika mchezo wa leo kwenye uwanja wa nyumbani na kuhakikusha wanapata ushindi dhidi ya Majimaji.

Ndayiragije alisema hawana budi kupambana hivyo hivyo ili kuhakikisha wanapata matokeo mazuri na kuzidi kujiweka vizuri kwenye msimamo wa ligi licha ya wachezaji wake kuchoka sana kutokana na safari ya umbali mrefu kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine kwa wiki moja kucheza mechi mbili za ligi.

Majimaji ambayo ilipata siku nane wa kuwepo Mwanza kuisubiri Mbao inaweza ikawa na nafasi kubwa ya kushinda leo kutokana na kupata muda mwingi wa kupumzika.

Mara ya mwisho ilicheza Februari 11 dhidi ya Stand mkoani Shinyanga, kisha ikatumia saa mbili tu kwenda Mwanza kuisubiri Mbao ambayo ilikuwa ikibadili mikoa tu kucheza mechi zake ndani ya wiki moja.

Mbao ilisafiri hadi Tanga kuifuata JKT Ruvu Jumapili iliyopita na kuambulia kipigo cha mabao 2-0 kisha ikasafiri kwenda Mtwara kucheza na Ndanda ambako nako ilikubali kichapo cha mabao 2-0 na Alhamisi ikaanza safari ya kurudi Mwanza ambapo leo itacheza na Majimaji.

Kocha wa Majimaji, Kally Ongala alisema wamejiandaa vizuri na wanachohitaji ni ushindi tu kwani wako katika nafasi mbaya kwenye msimamo wa ligi.

Kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona, Kocha wa Ndanda, Meja mstaafu Abdul Mingange anaamini mchezo wa leo dhidi ya African Lyon utakuwa mgumu kutokana na ubora wa wapinzani wao.

Hata hivyo, Mingange amesema ushindi wa mabao 2-0 ilioupata timu yake dhidi ya Mbao umeongeza morali kikosini hivyo na ana matumaini wachezaji wake wataendelea kujituma kupata ushindi mwingine utakaowafanya kupamda zaidi kwenye msimamo.

Mji Njombe yapanda Ligi Kuu Bara

Katika hatua nyingine, timu ya Mji Njombe ya Njombe imeungana na Lipuli ya Iringa na Singida United ya Singida kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.

Mji Njombe ilipata nafasi hiyo baada ya kuifunga Kurugenzi FC mabao 2-0 jana na kuifanya ifikishe pointi 22, zisizofikiwa na timu yoyote ya Kundi A.
Mpya zaidi Nzee zaidi