Hali ya sintofahamu imeibuka kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Gairo, baada ya mkuu wa wilaya hiyo Siriel Mchembe kususia baraza hilo na kuondoka bila kuaga,baada ya hoja aliyoitoa wakati baraza hilo likiendelea kushindwa kujadiliwa kwa madai hakupaswa kuchangia kwa vile hakuwa mjumbe halali wa kikao hicho.
Kuondoka kwa mkuu huyo wa wilaya bila kuaga katika kikao hicho,kumejitokeza baada ya awali kunyoosha mkono akiwa meza kuu na kupewa fursa ya kuzungumza wakati baraza hilo likiendelea kujadili bajeti ya mwaka wa fedha wa 2017/2018, ambapo alishauri bajeti hiyo kuzingatia vipaumbele ambavyo hakuviainisha,alivyodai kutolewa kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya kilichokutaka karibuni, lakini mwanasheria wa halmashauri hiyo mwongozo na mkurugenzi Agnes Mkandya, akadai kiongozi huyo hakupaswa kuchangia hoja kwavile hakuwa mjumbe halali wa baraza hilo na kama alikuwa na ushauri angeutoa kabla au baada ya kikao.
Wakichangia bajeti hiyo,madiwani wa halmashauri ya Gairo waliopitisha kwa kauli moja bajeti hiyo,wamedai imegusa maeneo yote ya vijiji,kata na halmashauri.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Gairo,Rachel Nyangasi, akabainisha mafanikio ya kukusanya shilingi bilioni 23.8 katika mwaka wa fedha wa 2017/2018,ikiwa ni asilimia 32 zaidi ya shilingi bilioni 17 za mwaka unaoishia, na hata kufikisha huduma kwa wananchi vitafanikiwa iwapo kutakuwa na usimamizi mzuri wa pande zote wakiwemo madiwani na wataalam.
