Simu zaleta mahitaji mapya kwenye mabasi ya abiria

Dar es Salaam. Awali mwonekano wa basi na nauli ndiyo vilikuwa vikipewa kipaumbele na abiria, pindi wafikapo kituo cha mabasi kwa ajili ya kusafiri.

Licha ya macho ya abiria kufanya kazi wapigadebe nao walikuwa wakiongeza chumvi kusifia gari husika, kwa sababu tu linaonekana kuwa katika hali nzuri.

Bila kujali mwendokasi au viburudisho vya ndani, jina na mwonekano wa gari vilitosha kumshawishi abiria kuingia kwenye basi tayari kwa safari.

Mabasi hasa yale yenye majina maarufu yalikuwa yakipeta kwa ule mtindo wa ‘kufanyia biashara jina’.

Mambo yameanza kubadilika sasa, kadiri teknolojia inavyokuwa abiria wamekuwa na mahitaji mapya katika magari wanayosafiria.

Kwa sasa ili basi liwe na uhakika wa abiria, ni muhimu ndani kuwe na kiyoyozi, mfumo wa kuchaji simu na mtandao wa intaneti.

Uchunguzi wa Mwananchi ulibaini hilo kwenye kituo cha mabasi ya kwenda mikoani na nchi jirani cha Ubungo jijini Dar es Salaam.

Katika uchunguzi huo mengi yalitajwa na abiria kama mambo wanayozingatia wanapochagua mabasi, ila suala zima la mawasiliano limeonekana kupewa kipaumbele.

Salim Kidenele alifika kituoni hapo kwa lengo la kutafuta usafiri wa kuelekea Tanga, lakini msisitizo wake ulikuwa kupata basi lenye mfumo wa kuchaji simu kwenye kiti atakachokaa.

“Unajua tunaotumia smartphone mara nyingi hazikai na chaji, wenye mabasi wameliona hilo na kuweka mfumo wa kuchaji simu kwenye viti,”

“Hivyo basi siwezi kupanda gari la kawaida nikapoteza mawasiliano njiani, wakati najua yapo mabasi yenye chaja kwenye siti itakayoniwezesha kuwa hewani siku nzima, ” alisema Kidenele.

Mambo yako tofauti kabisa kwa Oliva Ngalipa, kwake yeye basi zuri ni lile lenye mtandao wa intaneti utakaomuwezesha kuwasiliana muda wote wa safari.

Alisema huduma hiyo ndiyo kivutio cha kwanza anachopenda kukifahamu anapokwenda kituoni kukata tiketi.

“Mara nyingi napanda ‘luxury’, kwanza nataka nisafiri nikiwa kwenye basi la uhakika, nipulizwe na kiyoyozi, pili kwangu safari inakuwa nzuri ninapowasiliana sababu hiyo ndiyo inanifanya nichague gari lenye intaneti,” alisema.

Wakati hao wakionyesha kipaumbele chao kwenye simu Rakheem Mohamed ambaye ni wakala wa basi la Princess Muro alisema wapo abiria ambao hupenda kusafiri kwenye basi lenye kiyoyozi.

“Abiria wenyewe ndiyo wana uamuzi wa kuchagua ni basi lipi wapande kutokana na matakwa yao, wapo ambao wakifika jambo la kwanza kuulizia ni kiyoyozi kama hamna wala hashawishiki.”

Mohamed anabainisha kuwa mahitaji yote hayo yanatokana na daraja la gari ambalo abiria atachagua.

“Kila kitu kinapimwa na madaraja, yapo mabasi ya (daraja la kwanza) luxury, (daraja la pili) semi-luxury na (daraja la tatu) ordinary,”

“Utofauti upo kuanzia kwenye nauli, huduma zinazotolewa ndani ya basi, viburudisho na vikorombwezo vingine.”

Hilo linaungwa mkono na wakala wa basi la Machame Safari, Daud Francis ambaye anasisitiza kuwa abiria wengi wanafahamu mabasi wanayopanda.

Alisema, “Abiria wanajua wanataka basi gani, kuelekea wapi na kila mmoja ana vigezo vyake anapoamua kuchagua basi husika kulingana na mfuko wake.”
Mpya zaidi Nzee zaidi