China kuipiga jeki TTCL bil. 600/-

MAKAMU WA RAIS, SAMIA SULUHU HASSAN.

SERIKALI ya China ina mpango wa kuikopesha Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) Sh. bilioni 600 ili kuipa uwezo wa kiteknolojia na kupanua mtandao wa mawasiliano maeneo mbalimbali hasa vijijini.

Mbali ya hilo, serikali hiyo kupitia Shirika la Datang Telecom International Technology Company Limited, lina mpango wa kujenga kiwanda kikubwa cha kutengeneza vifaa vya mawasiliano Tanzania kwa kushirikiana na TTCL.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais ambayo Rais wa Shirika la Datang Telecom International Technology Company Limited la Serikali ya China, Yuan Yong, alimweleza nia hiyo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.

Taarifa hiyo ilimnukuu Yong alisema kuwa lengo la mkakati huo ni kuifanya TTCL kuwa kampuni bora inayotoa huduma za mawasiliano kwa njia ya kisasa kuliko kampuni yoyote katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Alisema mahusiano mazuri kati ya Tanzania na China, ndiyo yamepelekea shirika hilo kuweka mikakati ya kuja kuwekeza nchini katika sekta ya mawasiliano ili kuhakikisha wananchi wa Tanzania wanapata huduma bora za mawasiliano mijini na vijijini kwa njia ya kisasa bila usumbufu wowote.

Naye Makamu wa Rais, Samia alionyesha kufurahishwa na mikakati hiyo na kusisitiza kuwa serikali ipo tayari kwa uwekezaji huo mkubwa kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa pande hizo mbili.

Samia alisema ana imani kubwa kuwa uwekezaji huo ukikamilika, utaiwezesha (TTCL) kufanya kazi kwa ubora wa hali ya juu kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

Makamu wa Rais alisema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuelekea katika uchumi wa viwanda kwa kishindo, hali itakayosaidia taifa kuongeza pato lake la taifa pamoja na kutoa ajira kwa mamia ya wananchi kupitia viwanda ambavyo vitajengwa nchini.

Pia alipongeza mpango wa shirika hilo la Mawasiliano la Serikali ya China wa kutoa mafunzo mbalimbali kwa wafanyakazi wa TTCL ikiwamo ujenzi wa kituo kikubwa cha utafiti wa mawasiliano nchini hatua ambayo itasaidia kuimarisha utendaji kazi kwa wafanyakazi wa TTCL ili waendane na teknolojia ya kisasa ya mawasiliano duniani kupitia tafiti zitakazofanywa nchini.
Mpya zaidi Nzee zaidi