Hatimaye Temesa Yakabidhiwa Boti Nne Za Kisasa Baada Ya Ujenzi Wake Kukamilika

Boti tatu kati ya nne mpya zilizokabidhiwa leo kwa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) na Kampuni ya Songoro Marine Boatyard baada ya kukamilika kwa ujenzi wake. Makabidhiano yamefanyikia jijini Mwanza na boti hizo zitasafirishwa kuelekea Pangani Tanga, Kilambo Mtwara na Msangamkuu Mtwara ili zianze kutoa huduma kwa wananchi.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Dkt. Mussa Iddi Mgwatu, leo amepokea boti nne zilizokuwa zikijengwa na kampuni ya Songoro Marine Boatyard ya jijini Mwanza. Dkt. Mgwatu amesema kukamilika kwa boti hizi ni utekelezaji wa ahadi za Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Prof. Makame Mbarawa alizozitoa kwa wananchi wa Pangani Tanga pamoja na Kilambo na Msangamkuu Mtwara kwa nyakati tofauti.

Dkt. Mgwatu ameongeza kuwa boti hizo nne zitatoa huduma za dharura hasa wakati wa usiku kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa na pia kutoa usafiri mbadala wakati vivuko vikubwa vinapokuwa haviwezi kutoa huduma kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo kupungua kwa kina cha maji katika maeneo ya Kilambo mkoani Mtwara pamoja na Utete Mkoani Pwani.

Nae Mkurugenzi kutoka kampuni ya Songoro Marine Boatyard Mhandisi Major Songoro amesema kuwa boti tatu kati ya nne zilizokabidhidhiwa zimejengwa kwa kutumia “fibre Glass” na boti moja imejengwa kwa kutumia chuma. Boti ya MV Kuchele ambayo itapelekwa katika eneo la Msangamkuu Mtwara ina uwezo wa kubeba abiria nane, sawa na boti ya MV Bweni itakayopelekwa katika eneo la Pangani mkoani Tanga. MV Mkongo itakayopelekwa Utete mkoani Pwani ina uwezo wa kubeba abiria 40 na MV. Tangazo itakayopelekwa Kilambo/Namoto Mtwara ina uwezo wa kubeba abiria 25.

Aidha Dkt. Mgwatu ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa kuwezesha ujenzi wa boti hizo na tayari amemuagiza mkandarasi huyo kuhakikisha anazisafirisha boti hizo kwenye maeneo husika haraka iwezekanavyo ili wanachi waanze kunufaika na huduma mbadala itakayotolewa na boti hizo. Ujenzi wa boti hizo umefanywa kwa kutumia fedha za ndani na umegharimu jumla ya shilingi milioni 415.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items