Maswali 101 yatumika kuhoji utendaji wa Jeshi la Polisi

Dar es Salaam. Jukwaa la Haki na Usalama limezindua kitabu chenye maswali 101, yanayotoa uelewa kwa wananchi kuhusu utendaji wa Jeshi la Polisi nchini na wajibu wao katika kutetea haki.

Jukwaa hilo ambalo liko chini ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), limezingatia maswali mbalimbali ambayo wananchi wanapenda kujua, lakini wanakosa taarifa sahihi kutoka katika mamlaka zinazohusika.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mratibu wa jukwaa hilo, Stephen Msechu alisema kitabu hicho kimegusia maswali kuhusu dhana ya kuwa na jeshi hilo, haki na wajibu wa raia kwa polisi, taratibu za ndani ya polisi, demokrasia, utawala bora na uwajibikaji.

Msechu alisema katika kuandaa kitabu hicho, wameshirikisha wadau mbalimbali ikiwamo jeshi hilo, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB).

“Kitabu hiki kinalenga kujenga uhusiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi. Kila mmoja atambue haki na wajibu wake katika kutafuta haki. Kwa kuanzia tutasambaza nakala 3,000 nchi nzima,” alisema.

Kamishna wa THBUB, Dk Kelvin Mandopi aliwataka wadau kuhakikisha kuwa elimu iliyomo katika kitabu hicho inawafikia wananchi wengi.

“Tulipokea jambo hili na kutoa ushirikiano kwa waandaaji wa kitabu hiki ili kuhakikisha kwamba wananchi wanapata elimu sahihi, hasa kwa wanafunzi na polisi ambao ndiyo wanatekeleza sheria,” alisema.

Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria kutoka Wizara ya Sheria na Katiba, Justus Mulokozi alisema wanatambua juhudi za wadau katika kutoa elimu kuhusu masuala la kisheria na haki za wananchi.

Wakati huohuo, uongozi mpya wa TLS jana ulikwenda kujitambulisha kwa Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma ambaye aliwataka viongozi hao kuusoma na kuulewa mpango mkakati wa miaka mitano wa mahakama ya Tanzania ili waweze kuchangia katika utekelezaji wake.

Profesa Juma ni vyema viongozi hao wakausoma ili kufahamu mahakama inakotoka na inakokwenda, hususan katika suala la maboresho ya utoaji huduma.

Rais wa TLS, Tundu Lissu alimweleza Jaji Mkuu baadhi ya changamoto zinazowapata mawakili nchini ikiwamo baadhi ya mahakama kutokuwa na ofisi kwa ajili ya mawakili.

Akijibu hoja za Lissu, Msajili wa Mahakama Kuu, Ilvin Mugeta alisema wanaendelea kuzifanyia kazi changamoto zote wanazokutana nazo mawakili wawapo kazini.  
Mpya zaidi Nzee zaidi