Mgao wa Yanga wazuiliwa na mahakama

Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Kitengo cha Kazi imekubali ombi la Yanga la kuzuia fedha zake za mgao wa mapato ya mechi ya Simba na Yanga kulipwa kwa wadai wake Selestine Mwesigwa na Louis Sendeu.

Awali mahakama hiyo ilikazia hukumu kufuatia ushindi wa awali kutoka tume ya usuluhishi na uamuzi kwa kutoa maelekezo ya fedha za mgao wa mechi Simba na Yanga zilipwe kwa mmoja wa walalamikaji aliyekuwa Katibu Mkuu wa Yanga ambaye sasa ni Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Mwesingwa na aliyekuwa afisa habari wa Yanga, Louis Sendeu.

Kesi hiyo iliyoanza kusikilizwa mwaka 2012 , Sendeu na Mwesigwa wanaida Yanga Sh151 milioni ikiwa ni fidia ya kusitishiwa mikataba yao wakati huo wakiwa waajiriwa wa klabu hiyo.

Baada ya mkazo huo upande wa washtakiwa waliowakilishwa na mwanasheria Onesmo Mpinzile aliyeambatana na Mkuu wa kitengo cha fedha Baraka Deusdedit  jana hiyo waliwasilisha maombi ya dharura kuzuia utekelezaji huo wa malipo mpaka shauri hilo lisikilizwe upya ili walalamikiwa wajiridhishe juu ya mwenendo wa hukumu hiyo.

Kufuatia hukumu hiyo msajili wa mahakama hiyo alitoa maelekezo baada ya kusikiliza maombi hayo ya upande wa walalamikiwa kuzuia mgao huo wa Sh151 milioni na kuitaka Bodi ya Ligi Tanzania kupitia Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo Boniface Wambura kuzirudisha fedha hizo katika akaunti za Yanga.
Mpya zaidi Nzee zaidi