Azam yageukia Kombe la FA

Dar es Salam. Uongozi wa Azam umesema unaelekeza nguvu zao katika Kombe la Shirikisho (FA) ili ipate tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa mwakani.

Azam itashuka uwanjani kesho kucheza na Ndanda katika mchezo wa robo fainali ya FA kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Azam imeyasema hayo jana ilipotembelea makao makuu ya Benki ya NMB kukabidhi makombe kwa uongozi wa benki hiyo ambao ni wadhamini wa timu hiyo.

Mtendaji mkuu wa Azam, Saad Kawemba alisema timu yao imefanikiwa msimu huu kwa kutwaa makombe mawili.

“Tumechukua Ngao ya Jamii, Kombe la Mapinduzi na Mungu akijalia tutachukua na Kombe la FA maana katika Ligi Kuu nafasi yetu ya kuchukua ubingwa ni ndogo sana.”

“Tunawashukuru NMB kwa kuwa na sisi bega kwa bega na udhamini wao umetusaidia kuwa na timu sita huku tano zikiwa za vijana ambao baadaye wataichezea timu ya wakubwa na wengine hivi sasa ni msaada kwa timu ya Taifa,” alisema Kawemba.

Ofisa Mkuu wa Fedha wa NMB, Waziri Barnabas alisema huu ni msimu wa tatu wanaidhamini Azam wakiwa na lengo la kuifanya kuwa timu bora Afrika.

“Tunafurahia mafanikio yao na tuna matarajio makubwa kuwa itakuwa moja ya timu bora Afrika siku zijazo.” alisema Barnabas.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items