Hiki ndicho kinachowasibu Wafugaji

KATIBU MKUU WA CCWT, MAGEMBE MAKOYE.

CHAMA cha Wafugaji Tanzania (CCWT), kimesema kinajiandaa kwenda Dodoma kukutana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kumweleza adha na mateso wanayopata wanachama wake kwa kuhusishwa na migogoro kati ya wafugaji, wakulima na mamlaka za serikali.

Aidha, CCWT inasema migogoro mingi inachangiwa na baadhi ya watendaji wa serikali ngazi za vijiji na halmashauri kurubuniwa na wageni kwa kisingizio cha uwekezaji wa hoteli, mashamba makubwa na vitalu vya wanyama na uwindaji.

Katibu Mkuu wa CCWT, Magembe Makoye, alisema jana alipohojiwa na Nipashe maalum kuwa, migogoro inayoendelea kote nchini na kusababisha mauaji katika baadhi ya maeneo, imewasukuma kwenda kuzungumza na Waziri Mkuu.

“Kwa mfano hivi karibuni baadhi ya wanachama wetu wameondolewa kikatili katika maeneo yanayodaiwa .

Ni pori la akiba huko Karagwe mkoani Kagera bila kuambiwa waende wapi. Kama chama hatuungi mkono uvamizi wa mapori tengefu hasa unaofanywa na watu, lakini ni wazi kuwa wengi kati ya wanaofukuzwa na wafugaji wa Tanzania,” alisema.

Alisema wanataka kuonana na Waziri Mkuu ili kujadiliana kwa kina nafasi ya wafugaji katika nchi hii ambao wameifanya kuwa ya tatu kwa mifugo mingi Afrika, lakini hatma yao haieleweki kwa sababu hata viongozi wa wizara mama ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi hawaonyeshi kuguswa na mateso ya wafugaji.

Naibu Waziri wa wizara hiyo, William Ole Nasha, alisema wizara yake imejiwekea malengo matano makubwa kuhakikisha migogoro inakoma.

“Kwa sasa tumeanza kutafuta ardhi kwa ajili ya wafugaji pekee, ambapo tutailinda kisheria kwa kuweka miundombinu muhimu.

Pia tunafahamu jinsi ambavyo nchi ilivyoelemewa na wingi wa mifugo ambapo kuna mpango wa kutoa elimu na kuhamasisha watu kuwa na mifugo michache lakini yenye tija,” alisema.

Ole Nasha alisema ili kukabiliana na magomvi yanayoendelea wizara inawasiliana na nyingine za Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mambo ya Ndani ya Nchi na Ofisi ya Rais-Tamisemi ili kuja na mpango wa pamoja wenye tija na unaotekelezeka.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items