Kumbe Jiji la Dar lilitaka kuwa na eneo moja kuzikia

Dar es Salaam. Jiji la Dar es Salaam lilikuwa limeamua kununua eneo la kuzikia katika sehemu moja, lakini lilibadili uamuzi huo na kuelekeza mpango huo ufanyike kwa kila wilaya za mkoa huo.

Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita amesema baraza la madiwani limeshatenga Sh300 milioni kwa ajili ya kutafuta maeneo ya makaburi na kwamba, mpango huo utakamilika baada ya bajeti yao kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano.

“Makubaliano ya awali ilikuwa tutafute eneo moja la kuzikia katika wilaya fulani, lakini tumeona itakuwa shida kwa watu watakaokuwa wilaya za mbali. Tumekubaliana kununua viwanja vya makaburi katika wilaya zote. Kila kimoja kitakuwa na ukubwa wa eka kati ya 20 na 30,” amesema.

Mwita amesema hivi sasa wanasubiri bajeti ijadiliwe na kupitishwa na Bunge kisha irejeshwe katika baraza la madiwani.

“Bajeti ikisharejeshwa tutakaa na kamati ya fedha ili kujua tutaanza kununua eneo katika wilaya ipi. Kuna uwezekano tukaanza na Kinondoni lakini inategemea na wajumbe watakavyoamua,” alisema Mwita.

Baada ya bajeti kupitishwa mwezi uliopita, Mwenyekiti wa Kamati za Huduma za Jamii wa baraza hilo, Leila Hussein alisema hivi karibuni kuwa maeneo ya makaburi yatakayotengwa yatakuwa na huduma zote muhimu, ikiwamo sehemu ya kuandaa maiti kwa ajili ya maziko.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items