Mbao yaitambia Simba, yasema ijiandae kwa kimbunga

Dar es Salaam. Mbao FC wamesema baada ya Simba kukumbwa na dhoruba ya Kagera Sugar sasa wajiandae kukabiliana na kimbunga cha Mwanza.

Mbao watakuwa wenyeji wa Simba  Jumapili kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, mchezo utakaoamua hatima ya Simba katika mbio zake za kusaka ubingwa wa kwanza wa Ligi Kuu Bara baada ya miaka minne kupita.

Akiuzungumzia mchezo huo, kocha msaidizi wa Mbao, Bakari Best alisema wanataka kufuata nyayo za Kagera kwa kuifunga Simba katika mchezo wa Jumapili.

“Mzunguko wa kwanza, Simba ilitufunga bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa, tulifungwa kutokana na ugeni wetu katika ligi, lakini sasa ‘ushamba’ wa Ligi Kuu umeondoka, niseme tu baada ya kukumbwa na tetemeko la Kagera, wajiandae kukabiliana na kimbunga Mwanza,” alisema Best.

Akizungumzia maandalizi yao, Best alisema timu hiko sawa na kila mchezaji ana morali ya ushindi katika mchezo huo, ikasisitiza hawatakuwa tayari kufungwa nyumbani.

“Tunajua mchezo utakuwa mgumu, Simba inahitaji ubingwa, lakini sisi tunataka na sisi kuweka heshima nyumbani pia kujiokoa katika janga la kushuka daraja kwa kuwa ligi ilipofika hivi sasa ukizubaa umeachwa,” alisema kocha huyo.

Meneja wa Simba, Mussa Hassan Mgosi alisema kupoteza mchezo wa Kagera hakumaanishi kikosi chao ni kibovu na kusisitiza ligi bado haijaisha huku akiwasisitiza mashabiki kushtushwa na matokeo ya juzi.

“Tumepoteza pointi Kagera, mpira ndivyo ulivyo, tunajua tulikosea wapi na yaliyopita yamepita sasa tunaangalia mechi ijayo, tuko njiani tunakwenda Mwanza muda huu (jana saa tano asubuhi’), timu iko sawa na kocha ameona mapungufu yatafanyiwa kazi kwenye mechi ijayo,” alisema Mgosi.

Simba sasa ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 55 moja nyuma ya vinara Yanga 56 ambao wiki ijayo hawatakuwa na mechi wakicheza mchezo wake wa kimataifa dhidi ya MC Algers kusaka nafasi ya kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items