UVCCM yawashambulia wapinzani kuminya demokrasia uchaguzi Bunge la EALA

Kaimu Katibu Mkuu Taifa wa UVCCM,  Shaka Hamdu Shaka 

Dar es Salaam. Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) umeshangazwa na   mwenendo wa Demokrasia ndani ya vyama vya upinzani katika uteuzi wa kuwapata wagombea wa ubunge wa Bunge la Jumiya ya Afrika Mashariki (EALA).

Umoja huo umesema kuwa umesikitishwa na vyama vya Chadema, CUF na ACT-Wazalendo kwa kuwasilisha idadi ndogo ya wagombea katika Bunge hilo ambayo wamedai imetokana na uminywaji wa demokrasia ndani ya vyama hivyo.

Hayo yalisemwa jana na  Kaimu Katibu Mkuu Taifa wa UVCCM,  Shaka Hamdu Shaka alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mchakato wa uchaguzi wa ndani wa  umoja huo unaoanza leo.

Pia, alizungumzia suala la mtikisiko wa demokrasia katika mchakato wa uteuzi wa wagombea ubunge katika Bunge la EALA ulivyoendeshwa ndani ya vyama vya upinzani nchini.

Chadema kimewateua wanachama wake wawili, Ezekiah Wenje na Lawrence Masha kuwania nafasi hizo katika uchaguzi utakaofanyika Jumanne.

Kwa upande wa CUF wao wamemteua Twaha Taslima kuwania nafasi hiyo. na ACT-Wazalendo wamempitisha Profesa Kitila Mkumbo wakati CCM imepitisha wagombea 12.

“Tunakipongeza CCM na wanachama wake 450 walijitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi za ubunge EALA, lakini katu huu sio mwenendo mwema ulioonyeshwa na vyama vya upinzani.”

 Akijibu tuhuma za Shaka, Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano na Habari cha Chadema, Tumaini Makene alisema chama hicho hakina muda wa kufikiria maneno ya UVCCM kwa kuwa kwa sasa kinafanya kazi.

Uchaguzi ndani ya UVCCM

Umoja huo wa (UVCCM) umewaonya viongozi na wanachama wake kujiepusha na vitendo vya rushwa katika uchaguzi wa Jumuiya za CCM unatarajiwa kufanyika leo.

Shaka alisema tayari sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho imekamilisha uteuzi wa makatibu wa mikoa na wilaya katika jumuiya hiyo ambao watakuwa ndio wakurugenzi wa uchaguzi katika maeneo yao.

“Umoja wa Vijana wa CCM tayari umekamilisha maandalizi yote  kuhusiana na uchaguzi ikiwamo kusambaza vifaa katika mikoa na wilaya zote nchini. Vijana wajiepushe na vitendo vya rushwa au ukiukwaji wa maagizo na taratibu tulizojiwekea,”  alisema.

Aliongeza kuwa hawatamvumilia mtendaji yoyote atakayekiuka kanuni, taratibu na muongozo kwa makusudi ili kufurahisha kikundi au watu fulani.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items