Nimeumia sana kutolewa Kombe la FA: Manula

KIPA WA AZAM FC, AISHI MANULA.

KIPA wa Azam FC, Aishi Manula, amesema kuwa ameumia sana kuona timu yake imetolewa kwenye mashindano ya Kombe la FA na kuzima ndoto zao za kushiriki katika mashindano ya kimataifa yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) hapo mwakani.

Azam FC iliiaga michuano hiyo baada ya kukubali kufungwa bao 1-0 na Simba katika mechi ya hatua ya nusu fainali iliyofanyika juzi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kipa huyo alisema kuwa haikuwa dhamira ya wachezaji wa timu hiyo kupoteza mchezo huo, lakini kilichotokea uwanjani wanalazimika kukubaliana nacho.
"Kiukweli imeniuma sana, nguvu zetu zilikuwa zimebakia kwenye mashindano haya ili tuweze kupata tiketi ya kushiriki mashindano haya mwakani, tumeumia, sina lingine zaidi," alisema kipa huyo ambaye pia anaichezea Timu ya Taifa (Taifa Stars).

Naye Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Iddi Cheche, amesema hali ya mchezo kwa timu yake haikuwa nzuri na kadi nyekundu aliyoonyesha kiungo wake Salum Aboubakar 'Sureboy' katika dakika ya 16 iliwaondoka kwenye ushindani.

"Tangu tumetoka kambini kwetu hali ilikuwa hivi, wenyeji wa soka la Tanzania watakuwa wanajua, kadi nyekundu ya mapema ilitugharimu zaidi, iliharibu mipango yetu, tunarejea 'msituni' kwa ajili ya kusajili kikosi imara kwa ajili ya msimu ujao," aliongeza Cheche.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items