Mamlaka ya Mawasiliano nchini Rwanda (RURA) imeukosoa uamuzi uliotangazwa na Tume huru ya uchaguzi nchini Rwanda (NEC) kuhusu mpango wa kuizima mitandao ya kijamii katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa mkuu nchini humo.
Wiki iliyopita Rais wa NEC nchini Rwanda, Pro. Charles Mbanda, alisema wanafikiria kuhusu kuifungia mitandao ya kijamii kipindi cha uchaguzi mkuu unaokaribia ili isije ikatumiwa vibaya na kupelekea kuchochea vitendo vya uvunjivu wa amani.
Tamko hilo la NEC lilikemewa vikali na wachambuzi wa masuala ya kisiasa wakisema hatua hiyo inalenga kuwanyamazisha wapinzani.
Mwenyekiti wa Chama cha upinzani cha Democratic Green Party of Rwanda (DGPR), Frank Habineza, alisema hatua hiyo ni ya kuchukiza na anajiandaa kuishtaki NEC.
Hata hivyo Mamlaka ya mawasiliano nchini Rwanda (RURA) kupitia msemaji wake, Anthony Kulamba imewatoa hofu wananchi wa Rwanda kwa kusema kuwa NEC haina mamlaka ya kudhibiti matumizi ya mitandao ya kijamii.
Waziri wa mambo ya nje ya nchi nchini Rwanda, Bi Louise Mushikiwabo, amekemea uamuzi huo wa NEC akisema Wanyarwanda hawatakiwi kunyimwa uhuru wa kutoa maoni yao.
Awali Pro. Charles Mbanda alisema NEC itahitaji kuchunguza jumbe za wagombea urais kabla hawajazirusha mitandaoni huku akiwaonya kuwa kama watakaidi hatua za kinidhamu zitachukuliwa juu yao
Waziri Mushikiwabo ambaye ndiye msemaji wa serikali, amesema Wanyarwanda wanahitaji uhuru wa kujieleza na maudhui ya jumbe zao hayatakiwi kuchunguzwa namna hiyo.
