Jinsi Mchanga wa Dhahabu ulivyowavuruga Wabunge

Mvutano  wa aina yake ulianza majira ya saa nne asubuhi Bungeni Mjini Dodoma ,ambapo  wabunge walipokuwa wanajadili makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka ujao wa fedha.

Katika mjadala huo, watunga sheria hao waligawanyika katika pande mbili, mmoja ukiunga mkono hatua zilizochukuliwa na serikali kuzuia mchanga kusafirishwa nje ya nchi huku upande wa pili ukilalamikia kile ulichodai uamuzi huo haukizingatia hatua stahiki na utaligharimu taifa mabilioni ya shilingi.

Mvutano ulikolea zaidi majira ya saa sita mchana baada ya Mnyika kusimama na kukitaka Kiti cha Spika kuchukua hatua dhidi ya mbunge ambaye alisikika bungeni akitamka kuwa "Mnyika mwizi".

Wakati mchangiaji wa 16 jana, Livingstone Lusinde akichangia, Mnyika alisimama akisema "kuhusu utaratibu" na licha ya kutotaja kanuni husika, akilieleza Bunge kuwa Mbunge huyo wa Mtera (CCM) anapaswa kuacha kuwashambulia wapinzani kutokana na msimamo wao kuhusu makinikia kwa kuwa serikali ya CCM bado haijatangaza kuzuia usafirishaji wa madini kwenda ughaibuni.

Baada ya maelezo hayo, Mnyika aliketi na Lusinde akaendelea kuchangia huku akisema: "Ndiyo maana mimi huwa nasema wabunge tupimwe akili."

Wakati Lusinde akiendelea kuchangia, sauti ya mwanamke ilisika ikidai "Mnyika hana akili", jambo lililomwinua kitini mbunge huyo wa Kibamba (Chadema) na bila ruhusa ya Spika, alikitaka Kiti kichukue hatua dhidi ya mbunge huyo wa kike ambaye hakumtaja kwa jina, hata hivyo.

Spika alijaribu kumzimia kipaza sauti Mnyika lakini ilishindikana, hadi pale alipoomba msaada kutoka kwa wasaidizi wake.

Baada ya kufanikiwa kumzimia kipaza sauti mbunge huyo, Spika Ndugai alimwambia kuwa mbunge aliyekuwa ameruhusiwa kuzungumza na Lusinde na hakuwa ametamka maneno ya kumtusi Mnyika hivyo akamtaka Waziri Kivuli huyo kuketi.

Hata hivyo, Mnyika aliendelea kusimama na kulazimisha Kiti kichukue hatua dhidi ya mbunge mwenzake.

"Kwa mara ya mwisho, Mheshimiwa Mnyika nakuagiza uketi chini," alisikika Spika Ndugai kisha akaagiza askari wa Bunge wamwondoe ukumbini mbunge huyo kutokana na kukaidi agizo lake.

"Leo (jana) ni Ijumaa, huyu asionekane hapa bungeni kwa wiki nzima," alisema Spika Ndugai.

Baada ya agizo hilo, askari watatu walienda alipokuwa amesimama Mnyika na kumwomba atoke ndani ya Bunge lakini akawa anawaangalia tu bila kutii maagizo yao.

Kutokana na hali hiyo, Spika Ndugai alisikika akifoka 'Nyie askari au raia, toeni huyo hadi nje kabisa ya geti la Bunge."

Kauli hiyo ya Spika ilifuatwa na kundi kubwa la askari ambao walizunguka na kumtoa kwa nguvu bungeni mbunge huyo.

Wakati Mnyika anatolewa ukumbini, Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya (Chadema), akiwa nyuma ya askari, alimsindikiza hadi kwenye lango kuu la kuingia ukumbini kisha akarejea na akaonekana akiwaonyesha ishara wabunge wa upinzani waondoke ukumbini.

Wabunge wote wa upinzani waliokuwamo ukumbini walitii agizo hilo la Bulaya isipokuwa Maftaha Nachuma (Mtwara Mjini-CUF).

Nje ya Ukumbi wa Bunge, Bulaya aliwaambia waandishi wa habari kuwa waliamua kutoka ukumbini kutokana na Kiti cha Spika kutotenda haki.

"Tulitarajia kuona Spika akimuonya mbunge aliyemtukana Mnyika. Wabunge wa upinzani wakifanya kosa, wanaadhibiwa, kwanini CCM hawaadhibiwi?" alihoji.

"Mbona bajeti ya Wizara ya Ardhi tuliiunga mkono na ilipita bila kupingwa? Mikataba mibovu kwenye madini tumelipigia kelele kwa muda mrefu, leo tunaambiwa tumehongwa."

Kabla ya kusitisha shughuli za Bunge jana mchana, Spika Ndugai alizungumzia adhabu aliyoitoa dhidi ya Mnyika huku akieleza kuwa chombo hicho cha kutunga sheria kiko imara.

"Nataka niwahakikishie Watanzania, Bunge hili ni imara na kazi ya kupitia bajeti ya serikali tutaifanya mpaka mwisho na serikali itapata bajeti yake na utekelezaji utaanza kwa tarehe zilivyopangwa," alisema.

"Kwa hiyo, bado tupo kwenye reli kabisa, haya mambo madogomadogo ni changamoto za kawaida ambazo lazima tupambane nazo."

Alisema aliamua kumwadhibu Mnyika kutokana na mbunge huyo kudharau mamlaka ya Kiti na kufanya vurugu bungeni.

"Nianze kwa nini nimempa adhabu Mheshimiwa Mnyika pamoja na kile ambacho wote mmekishuhudia. Mbunge yeyote unaposimama kusema kuhusu utaratibu, maana yake unatumia Kanuni ya 68(1),(2) na (3).

"Kanuni (kifungu) ya pili inasema mbunge anayedai utaratibu, atalazimika kutaja kanuni au sehemu ya kanuni iliyokiukwa, ya tatu inasema baada ya kutaja kanuni au sehemu kanuni iliyokiukwa, mbunge aliyesimama kuhusu utaratibu, ataketi mahali pake kusubiri maelekezo na uamuzi wa Spika.

"Mtaona toka mwanzo, kikanuni sikutaka kumbana kikanuni kwa sababu alikuwa yupo nje kabisa mpaka sasa hivi nikiwauliza ni utaratibu upi alikuwa akizungumzia au kanuni ipi katika kanuni zetu zote hizi aliyokuwa anadai imevunjwa, hutaweza kuipata.

"Lakini kubwa zaidi alikuwa ni mtu anayeleta fujo kubishana na Spika kwa kiwango ambacho hakiwezi kuvumilika na ndiyo maana nimempa adhabu hiyo ya kutohudhuria vikao wiki nzima.

"Nilimsikia kwa mbali kuwa atakata rufaa, mwacheni akate rufaa, tunasubiri sana ujuaji huo lakini kama niliposema mwanzo, msiwe na wasiwasi."

BULAYA KIKAANGONI
Spika Ndugai pia alisema wakati fujo zikitokea, Bulaya alikuwa akizunguka ukumbini na kufanya fujo ambazo alidai ni aibu kwa wananchi wa Bunda na wanawake nchini.

"... maana wanawake zetu hawafanani hivi, amefanya vitu vya ajabu sina haja ya kuvisema mapema kwa sababu nimeshampeleka kwenye Kamati ya Maadili na nataka Kamati ya Maadili mchana huu mkutane katika ukumbi wenu kuweka utaratibu kuanzia kesho (leo) asubuhi huyo Mheshimiwa aitwe katika kikao chenu na barua yake ya wito apate leo (jana) ili asije akatoroka hapa mjini," alisema.

"Na hata kama atatoroka, kikao kiendelee kama kawaida na Jumatatu asubuhi, tunaanza na adhabu hiyo.

MDEE NA SARE YA ASKARI
Aidha, Spika Ndugai aliitaka kamati hiyo kutafakari azimio la Bunge la kumsamehe Halima Mdee licha ya kupendekezwa awali achukuliwe hatua ya kuzuiwa kuhudhuria vikao vyote vya mkutano wa Bunge la Bajeti baada ya kutukana bungeni Aprili 4 wakati wa uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) akidai kuwa jana mbunge huyo wa Kawe (Chadema) alimchania koti askari bungeni.

"Lakini wakati askari wanamtoa Mnyika, Halima Mdee alikuja akavamia askari akawa anavuta koti la askari ili kumchania askari koti lake, ni jambo ambalo ni aibu kubwa kwa mbunge kufanya," alisema.

"Kwa hiyo huyu naye tunaikumbushia Kamati ya Maadili adhabu yake ambayo ilikuwa inasema Kiti ningeweza tu kumaliza hapa lakini nataka wanishauri kwa kitendo kama hiki adhabu iliyopendekezwa wakati ule inatosha na yeye Jumatatu hapa asubuhi tunaanza nao, yaani Jumatatu hawa tunaanza nao."

MOTO WA MAKINIKIA
Akizungumzia kuhusu makinikia, Spika Ndugai alisema hatua alizozichukua Rais zinaungwa mkono na Bunge na ndiyo mama yeye mwenyewe aliona uzito wa jambo hilo na kuamua kwenda bandari kuangalia mchanga huo.

"Kama mnavyofahamu Spika hajawahi kutoka kwenda kwenye jambo lolote la mradi au kukagua chochote na nyie mnafahamu lakini kwa hili, niliondoka mimi mwenyewe hadi bandarini na kuna baadhi ya wabunge nilienda nao," alisema.

"Kwa uzito wake, hili jambo ni jambo kubwa na siyo jambo dogo hatuwezi Watanzania tukawa tunaibiwa tunachekacheka, haiwezekani na tunajua katika nchi hii na baadhi ya wabunge hapa huwa wanasimama 'ku-retailer impressets'.

"Hawezi mtu akasimama kuwashabikia watu wanaoitia hasara nchi yetu kiasi hicho na yeye ni mbunge, anatoka kwenye jimbo ambalo madarasa hayatoshi vyumba, vyoo, madarasa, idadi ya walimu, barabara, zahanati hazitoshi, dawa... fedha zinapotea halafu mbunge huyohuyo anaunga mkono jambo hilo.

"Ukiona mbunge anafanya hayo, jua kuna mshindo nyuma, kitu fulani, hiyo ndo namna ya kuona sasa mngejuaje si ndiyo muone. Wizara ya Nishati na Madini muwe mnajua wanaosimamia bajeti yenu mpaka mwisho ni kina nani hasa.

"Nnyie tatizo lenu nini? Sihitaji kusema hapa kama ni mpira si unajua pasi unapiga upande gani, piga pasi inavyotakiwa utaona mwakani watu wamekaa hapa, hii huruma yenu ndiyo inaleta matatizo, amekupitishia bajeti mwingine, unashughulika na mwingine na wananchi wakiuliza jibu unalo mbunge wao alikataa kupitisha bajeti, si basi.

"Hivi wewe bajeti ya (WIzara ya) Nishati na Madini unatoka nje, we mbunge una akili" Halafu unategemea wananchi wako itakuwaje?" alihoji.

DALILI YA MVUA MAWINGU
Kutokea kwa mvutano katika mjadala huo kulianza kuonekana mapema jana asubuhi wakati wabunge walipoanza kuchangia.

Mbunge wa kwanza alikuwa Hamidu Bobali (Mchinga-CUF) ambaye aliitaka serikali kuwaomba radhi Watanzania kwa kuwafanya kuwa maskini ilhali nchi ina madini yanayonufaisha wawekezaji.

Bobali pia alidai wananchi wa jimboni kwake hawajashirikishwa katika utafutaji na uchimbaji wa madini unaoendelea.

Mchangiaji wa pili alikuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema), ambaye hakuzungumza chochote kuhusu wizara hiyo baada ya Spika Ndugai kumtaka kuketi kutokana na kutumia muda mwingi kumshambulia kwa maneno Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, akidai waziri huyo hakutenda haki kumtuhumu kuingia na chupa ya kilevi bungeni hivi karibuni.

Baada ya Nassari kuzuiwa, Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema), alipewa nafasi ya kuchangia lakini alilazimika kuketi kupisha kupewa taarifa na Joseph Musukuma baada ya kudai kuwa mbunge huyo wa Geita (CCM) anahitaji kupimwa matumizi ya dawa za kulevya.

Katika maelezo yake, Waitara alimshangaa mbunge huyo kwa kudai kuwa wabunge wa upinzani wamehongwa.

Akimpa taarifa Waitara, Musukuma alisema anajua kuna baadhi ya wabunge wamehongwa huku akitishia kuwataja, lakini hadi anaketi, hakutaja jina la mbunge yeyote.

Mbuge wa Ulanga, Goodluck Mlinga (CCM), aliwatuhumu wabunge wa upinzani kutumika akidai wamehongwa na wazungu.

Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja (CCM), alilishauri Bunge liazimie kufanya mapitio ya sheria zote za madini kwa kuwa hazijawahi kufanyiwa marekebisho kwa miaka saba sasa.

Tuache kunyoosheana vidole, Kifungu cha 11 cha Sheria ya Madini kinataka mikataba yote ya madini ifanyiwe 'review' (mapitio) kila baada ya miaka mitano lakini sasa ni miaka saba hatujafanya hivyo," alisema huku akishangiliwa na wabunge wa vyama vyote.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items