MENEJA wa Ardhi wa mgodi wa Acacia North Mara, raia wa kigeni aliyetambuliwa kwa jina la Peter Enger juzi alikamatwa kwa amri ya mkuu wa mkoa, baada ya kampuni hiyo kushindwa kulipa wananchi fidia kwa miaka mitatu
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorius Luoga alisema alifikia uamuzi wa kuamuru Enger akamatwe kama suluhisho la malipo ya fidia kwa wananchi.
Zaidi ya wakazi 1,000 wanaodai fidia za mali zao, yakiwamo mazao na nyumba kutoka katika vitongoji vya Nyamichele, Muryambai na vijiji vya Kewanja, Matongo, Kerende, Nyakunguru na Nyamwaga waliandamana juzi mpaka kwenye lango kuu la mgodi wa North Mara.
Walikuwa wakishinikiza kulipwa fidia na mgodi huo kama ulivyoahidi na kusisitizwa na serikali ya wilaya katika siku za nyuma.
Luoga alisema aliagiza meneja huyo akamatwe na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi Musoma, baada ya kufika mgodini hapo kutuliza waandamanaji hao.
"Tumefanikiwa kuzima maandamano haya na kuwaomba wananchi kwa wale waliokwishafanyiwa tathmini za mali zao, yakiwamo mazao na nyumba wawe na subira," alisema Luoga.
"Hata sisi serikali hatuoni vyema kampuni hii ya Acacia North Mara kusuasua kulipa fidia kwa wananchi kwa zaidi ya miaka mitatu."
Malipo ya fidia hiyo kwa wananchi ambayo Nipashe haikuweza kupata kima chake mara moja, awali yalichelewa kutokana na madai ya kuwapo kwa majina hewa, lakini serikali iliingilia kati na kuyaondoa.
"Nimeagiza kushikiliwa kwa meneja huyu wa Kitengo cha Ardhi na Fidia Peter Enger kwa mahojiano zaidi," alisema Luoga.Luoga aliwataka wananchi kuwa watulivu na kusubiri malipo yao.
"Tunahimiza mgodi kuwalipa fidia wale wanaostahili kulipwa ambao majina yao hayana mgongano wala mashaka."Enger hakuweza kuzungumza lolote na waandishi wa habari mgodini hapo kwani alikuwa chini ya ulinzi kutokana na wananchi kujawa na hasira dhidi ya kampuni hiyo ambayo wanadai imewakwamisha kimaendeleo.
Wananchi hao walisema Acacia imewafanya washindwe kulima mashamba yao yaliyochukuliwa na kufanyiwa tathmini na mgodi huo kwa zaidi ya miaka mitatu.
WAKATI MGUMUAcacia pia ipo katika wakati mgumu kwa sasa baada ya kamati iliyoteuliwa na Rais Magufuli Machi 29, ikiwa na wajumbe nane wenye taaluma za jiolojia, kemia, uhandisi kemikali na uhandisi uchenjuaji madini, kuchunguza kiwango cha mali kwenye makinikia kuonyesha kuwapo kwa udanganyifu.
Miezi miwili iliyopita, Rais Magufuli alizuia makontena 277 ya mchanga wa madini (makinikia) ya Acacia na wafanyabiashara wengine yaliyokuwa yanasafirisha kwenda kuchenjuliwa ughaibuni kisha akaunda kamati mbili za kufuatilia kilichokuwamo baada ya baadhi ya wataalamu kudai kulikuwa na kiasi kikubwa cha dhahabu ndani yake.
Baada ya kamati ya kwanza kumkabidhi ripoti ya uchunguzi wiki Mei 24, Rais Magufuli alichukua uamuzi wa kusitisha upelekaji mchanga nje ya nchi mpaka itakapoelezwa vinginevyo baadaye.
Aidha, Rais Magufuli aliwawajibisha baadhi ya watendaji wa serikali ikiwamo kutengua uteuzi wa Prof. Sospeter Muhongo katika baraza lake la mawaziri.
Kamati hiyo maalumu iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Profesa Abdulkarim Mruma, ilionyesha nchi imekuwa ikipoteza wastani wa kati ya Sh. bilioni 829 mpaka Sh. trilioni 1.44 kwa mwezi katika usafirishaji wa mchanga wa dhahabu unaokwenda kuchenjuliwa nje ya nchi.
Mgodi wa North Mara upo Nyamongo wilayani Tarime mkoani Mara
