Madiwani Nachingwea waliamsha, wataka umiliki wa jengo

Ahmad Mmow, Nachingwea.
MADIWANI wa halmashauri ya wilaya ya Nachingwea, jana walifufua upya dai lao la muda mrefu la kutaka atambulike mmiliki wa jengo lenye  ofisi za mkuu wa wilaya  na halmashauri hiyo linalotambulika kwa jina la Boma. Hayo yalijiri jana wakati wa kikao cha baraza la madiwani wa halmshauri hiyo.

Ikiwa ni cha robo ya nne ya mwaka wa fedha wa 2016 /2017, kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya wilaya, mjini Nachingwea. Aliyeibua hoja hiyo kwenye kikao hicho kilichokuwa na agenda 12, ni diwani wa kata ya  Mkotokuyana, Saada Makota (CCM). Makota alisema imefika wakati wa kutambuliwa mmiliki wa jengo hilo lenye ghorofa moja na vyumba takribani 70, ninani baina ya serikali kuu na halmashauri ya wilaya hiyo.

Akiweka wazi kwamba ukweli huo utarejesha imani kwa wananchi ambao nguvu zao na mali vilitumika kwa ujenzi wa jengo hilo linalotumiwa na halmashauri ya na mkuu wa wilaya. Kwani wote ofisi zao zipo kwenye jengo hilo. Kauli ya Makota iliungwa mkono na diwani wa viti maalumu (CCM) Joyce Ntauka, aliyesema kutofahamika mmiliki halali baina ya halmashauri na serikali kuu kunasababisha wananchi kuanza kukata tamaa ya kuchangia shuguli nyingine za maendeleo. Hata kama wakiambiwa ni kwa faida yao na mali yao.

Kwamadai kuwa wanaogopa kunyang'anywa umiliki kama inavyotaka kufanyika kwa jengo hilo ambalo ujenzi wake kwakiasi kikubwa ulitokana  na nguvu za wananchi. Ikiwamo fedha na vifaa vya ujenzi. "Kama ni uzalendo basi waheshimiwa madiwani wenzangu tuoneshe katika jambo hili. wananchi wanahoji na kuuliza kuhusu jambo hili," alisema Ntauka. Diwani huyo alisema umefika wakati wa kutafuta na kuandaa historia ya jengo hilo ili ukweli uwekwe wazi na apelekewe waziri mwenye dhamana ili mwenye haki aweze kumilikishwa.

Diwani wakata ya Kilimani hewa Rashid Michinge ( CCM) alisema kutokana na umuhimu wa jambo hilo iundwe kamati  na iagizwe kufanya kazi ya kutafuta ukweli utakaoonesha ukweli wa  nani ni mmiliki halali.huku Huku Joyce Makota (viti maalum CCM) akihimiza mchakato wa kuundwa kamati ndogo itakayo shugulikia suala hilo iundwe haraka. Huku akimuomba mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Ahmad Makoroganya aunde kamati hiyo ili ukweli uwekwe wazi ili mwenye haki apewe. Nae diwani wa Mnero Ngongo, Hamisi Mbinga (CHADEMA) alisema kuna kila sababu ya jengo hilo kufahamika mmiliki wake. Badala ya kuendelea na hali hiyo wakati kwenye kata zao wanalaumiwa na wananchi.

Ambapo  diwani wa kata ya Boma, Hamisi Kambona akisema ujenzi wa jengo hilo hauna utata wowote kiasi cha kutafuta ukweli. Kwamadai kwamba inafahamika na kueleweka kuwa wananchi waliufanya. Baada ya madiwani hao kueleza hayo ndipo mwenyekiti wa Halmashauri, hiyo, Ahmad Makoroganya  alipogongea msumari maelezo ya madiwani hao mbele ya mkuu wa wilaya hiyo, Rukia Muwango, ambae alikuwepo ukumbuni humo.

Makoroganya alisema anajua chanzo cha jambo hilo na kitu gani kimesababisha kufika hapo. "Ninajua jambo hilo liliharibikia wapi, hivyo lazima tuanzishe hiyo hoja. Hata mkuu wa wilaya anajua msimamo wangu kuhusu jambo hili, nimemwambia kuwa jengo hili ni mali ya halmashauri, lazima tuseme," alisisitiza Makoroganya. Mkuu wa wilaya hiyo, Rukia Muwango ambae wakati wa mjadala huo alionesha utulivu wa hali ya juu, licha ya kusema hakuwa na sababu ya kulizungumzia jambo hilo ambalo limewahi kuzungumzwa na viongozi wake.

Alisema yeye anachoangalia na kujali nikutimiza wajibu wake wa kuwahudumia wananchi ili wapate maendeleo. Kwani hilo ndilo wanalohitaji. Sio atawahudumia akiwa amekaa ofisini ama chini ya mti, bali atimize wajibu wake kikamilifu na ufanisi mkubwa." Kuhusu jengo sitaongelea, nahisi kunatafutwa mimi kufukuzwa tu. Mimi ninachojali ni kuwatumikia wananchi sio nafanyia wapi, tunachohitaji nikuwapelekea maendeleo, "alisema Muwango.

Hata hivyo baada ya kauli hiyo Makoroganya alichomeka kauli na kusema :" Kinachotafutwa sio kumfukuza mkuu wa wilaya. Kwanza wewe wala mwenzako aliyetangulia hamuhusiki. Ila hata wewe unaweza kuwa msaada katika jambo hili iwapo utasema ni kweli jengo hili ni mali ya halmashauri ya wilaya, "Makoroganya alizidi kuweka chumvi kwenye kidonda. Mbali na hayo mwenyekiti huyo alisema katika mwaka wa fedha wa 2016/2017, halmashauri hiyo imevuka lengo la makisio ya kukusanya fedha zinazotokana na vyanzo vyake vya ndani.

Ambapo imeweza kukusanya takribani shilingi 2. 997 bilioni. Sawa na asilimia 100. 5. Wakati makisio yalikuwa shilingi 2.8 bilioni. Hii sio mara ya kwanza kutokea mvutano kuhusu umiliki wa jengo hilo. Bali umekuwa ukitulia na kuanza upya.


Mpya zaidi Nzee zaidi