HALMASHAURI ya jiji la Dar es Salaam imepata hati safi kupitia taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2015/2016.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa mara baada ya kumalizika kwa baraza la madiwani la halmashauri ya jiji iliyokuwa na ajenda moja ya kuwasilisha taarifa ya CAG, Mstahiki Meya Isaya Mwita alisema kuwa hati hiyo imetokana na kuwepo kwa usimamizi mzuri wa matumuzi ya fedha.
Wakati huo huo ,Meya Mwita alisema kuwa jiji limetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya kununua maeneo ya makaburi kutokana na kuwepo kwa changamoto ya maeneo ya kuzikia watu.
Alisema kwasasa hali imekuwa mbaya kwenye maeneo ya jiji na kwamba pesa hizo zitatumika kununua maeneo ambayo yatatumika kwa ajili ya kuzikia watu wanapopoteza maisha.
“ Jambo hili litaanza kufanyika mwaka huu, kila halmashauri itapatiwa eneo kwa ajili ya kuzikia watu, yapo maeneo ambayo tumepanga kuyanunua, ukiangalia jiji letu lina watu wengi sana, kadiri siku zinavyozidi kwenda ndivyo watu wanavyozidi kuongezeka.
Leo hii imefikia hatua mtu ana zikwa juu ya mtu mwingine, jambo hili sio zuri, hata wandishi wa habari leo nikiwaualiza akifa mtu hapa anazikwa wapi, hakuna sasa utekelezaji wa jambo hili utaanza kufanyika mwaka huu” alisema Meya Mwita.
